NA MWANDISHI WETU, KATAVI
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Magharibi kimeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuboresha mazingira ya kufanya siasa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Magharibi, Mussa Katambi wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho katika ukumbi wa Usiga uliopo mjini Mpanda Mkoa wa Katavi.
“Tumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa sasa (Rais Samia Suluhu Hassan), wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, anaendelea kuboresha mazingira ya kufanya siasa,” amesema.
Amesema, kuboreshwa kwa mazingira ya siasa ni wakati sasa kwa wanachama wa chama hicho wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kujitokeza, ikwemo kuweka mikakati ya kushinda majimbo yote ya Mkoa wa Katavi.
Katambi amesema chama hicho Kanda ya Magharibi kimefungua milango kwa wafuasi wa vyama vingine na wote waliokimbia kurudi kundini, ili kuendeleza mapambano ya chama hicho.
Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Katavi, Almas Ntije amesema awamu hii hawatasusia uchaguzi na badala yake watashiriki chaguzi zote na hadi sasa wanaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.
Katibu wa wanawake CHADEMA Mkoa wa Katavi, Neema Elias ametoa wito kwa wanawake wote mkoani humo kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali bila woga.