Na Mwandishi Wetu
-SAME
MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amewaonya viongozi na wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya Serikali na kujimilikisha au kufanya shughuli zozote za Maendeleo.
Ametoa onyo hilo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kata za Vunta na Myamba ambapo amesema katika maeneo hayo kumekuwa tabia ya baadhi ya watu kuvamia na kulima ama kujenga katika maeneo ya Serikali.
“Ofisa Tarafa hakikisha unakagua maeneo ya Serikali na iwapo utabaini Kuna uvamizi wowote hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika,hatuwezi kuvumilia kuona maeneo ya Serikali yanachukuliwa hovyo hovyo”alielekeza Kasilda.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuungana kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo na nchi kwa ujumla.
Katika ziara hiyo kuna baadhi ya wananchi walilalamikia kutolipwa fedha zao baada ya kumuuzia kokoto Mkandarasi wa kampuni ya (Nure Building & Civil Contractors) anayejenga barabara ya Hedaru- Vunta, Mamba Myamba ambapo DC amemuagiza mkandarasi huyo kuwalipa fedha zao wananchi hao ili kuondoa malalamiko hayo na kuwawezesha kujenga Imani kwa makampuni yanayofika kutoa huduma Vijijini.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Vunta Mongera Kanyika amemshukuru Mkuu wa Wlaya kwa kuendelea kutatua kero mbalimbali zilizopo katika Kata hiyo na pia kuwahamasisha wananchi wa Kata ya vunta kujikita kwenye kilimo cha parachichi kutokana na rutuba nzuri ya ardhi yao.