Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
Mwanasheria Jonathan Mdeme, aliyekuwa akimwakilisha mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Bernard Membe (69) kwenye kesi dhidi ya mwanahabari Cyprian Musiba, amesema deni la waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje kwa Musiba liko palepale na msimamizi wa mirathi ataendelea alipoishia.
Membe ambaye aliwahi kuhudumu kama waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, amefariki leo Ijumaa Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Kairuki iliyopo Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu.
Oktoba 28, 2021, Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ilimuamuru Musiba anayejitambulisha kama mwanaharakati huru kumlipa Membe fidia ya Sh bilioni 6.
Kesi hiyo namba 220 ya mwaka 2018, Membe alimdai Musiba fidia ya Sh bilioni 10.3 kwa madai ya kumkashfu kupitia magazeti yake ya Tanzanite.
Akizungumza leo Mei 12, 2023 kuhusu hatima ya deni hilo, Wakili Mndeme amesema madai dhidi ya Musiba hayatafutika kwa sababu msimamizi wa mirathi ataendelea kufuatilia madeni ya marehemu.
“Katika makosa ya jinai, mtuhumiwa akifariki kesi inaisha hapo, katika makosa ya madai ni tofauti. Anateuliwa msimamizi wa mirathi ya marehemu halafu anavaa viatu vya marehemu kukusanya madeni na mapato kama yapo.
“Kama madeni yanalipwa, kama ni mapato yanagawanywa kwa mrithi halali kwa maana mke na watoto. Kwa hiyo kesi ya madai dhidi ya Musiba ni shauri la madai hivyo halitafutika kwa sababu msimamizi wa mirathi ataendeleza pale alipoishia,” amesema
Mndeme amesema kesi iko katika hatua ya kukazia hukumu au utekelezaji wa hukumu na maombi yaliwasilishwa mwaka 2022 na kupewa namba 26 ya mwaka 2022 na Mahakama ya Kuu Dar es Salaam.
Wakili huyo wa Membe amesema mara baada ta kumalizika kwa kesi hiyo tayari alishateuliwa dalali kuendelea na kazi kukazia hukumu.
Akizungumzia kifo cha mteja wake huyo, Mndeme ameeleza kusikitishwa akisema alikuwa ni mtu mwenye msimamo na kujiamini.
“Mimi sijapoteza tu mteja, bali nimepoteza rafiki yangu na jana nimezungumza naye na kushauariana naye mambo mengi.
“Nimejifunza kufanya kazi na mtu aliyefanya kazi serikalini. Kujiamini na kusimamia msimamo, ukitaka kufanya jambo unalifanya kwa kujiamini na mteja wangu alikuwa anajiamini na kuendesha kesi miaka mitatu katika mazingira magumu,” amesema Wakili Mndeme.
Amesema Membe alikuwa mtu anayepokea ushauri na kwamba hakuwa mbishi na kwamba alikuwa na uwezo na mwenye kumbukumbu sawia na uelewa mkubwa.