Na Mwandishi Wetu
-Dar es Salaam
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake imeanza mazungumzo kwa ajili ya ujenzi wa satellite nchini.
Hayo ameyasema leo Alhamisi Mei 18, 2023 katika uzinduzi wa mradi wa minara ya kurusha matangazo ya Televisheni ardhini (DTT) inayomilikiwa na kampuni ya Azam Media Limited.
Ikiwa mpango huo utakamilika ni wazi sasa Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za Afrika zilizofanikiwa kupeleka kifaa hicho angani, ambapo nchi hizo ni Algeria, Ethiopia, Kenya, Zimbabwe, Afrika Kusini, Morocco, Misri, Ghana na Nigeria, huku Rwanda ikikusudia kufanya hivyo mwishoni mwa mwaka huu.
Pamoja na hali hiyo Mkuu huyo wan chi, ni wazi alionekana kutofurahia ujenzi wa minara ya mawasiliano unaoendela nchini huku akishauri kuangaliwe namna bora ambayo nchi inaweza kukusanya mambo yote kwa pamoja bila kuwa na mambo mengi.
“Tatizo nililonalo kichwani kwangu ni moja, nikamuambia Waziri, minara 758 mipya, kuna minara ambayo tayari ipo ndani ya nchi, kuna minara ya Azam Media itakwenda kujengwa na wengine watakuja na minara,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo Rais Samia, amesema kuwa uwepo wa minara mingi ilimfanya kumhoji Waziri mhusika ili kujua kama kunawezakuwa na teknolojia mbadala.
“Nikamuuliza Waziri hakuna teknolojia ya kuchanganya haya yote yakaingia sehemu moja, kwa sababu nchi yote itajaa minara, kila utakapokwenda minara, minara, ukiuliza huu wa wa Azam, Tigo na huu wa Voda, nchi yote itajaa minara,” amehoji Rais Samia.
Licha ya hali hiyo amesema kuwa ni vyema kama nchi ikatafuta teknolojia itakayoweza kuchanganya vyote kwa pamoja.
“Najua kama Serikali tunajipanga kuja na setelaiti ambayo niwahakikishie kuwa itakuwepo Tanzania, tunajipanga vizuri tumeanza mazungumzo tutajenga setelaiti Tanzania.”
Rais Samia, amesema wakati hilo likifanyika ni vyema kuangalia namna ya kukusanya mambo yote na nchi ikapata huduma zote kwa moja bila ya kuwa na mambo mengi yamesimama.
“Wote tunakumbuka kuwa nchi yetu iliachana na mfumo wa analojia katika matangazo ya Televisheni na kutumia teknolojia ya digitali tangu Juni 17, 2015, hatua hii ilikuwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa kutokana na faida nyingi kama vile ubora wa picha na sauti matumizi bora ya masafa ya utangazaji, na nishati ya umeme.
“…. uwezekano wa kutoa huduma za ziada kama internet na matumizi ya runinga za mkononi na kwenye magari, Tanzania ilifanikisha mpango huu ndani ya muda uliopangwa,” amesema Rais Samia.
Mazingira wezeshi
Mkuu huyo wan chi, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kuhakikisha uendelevu wa sekta ya habari kwa upande wa teknolojia ya utangazaji.
“Na nimejulishwa kuwa mwaka 2021, Wizara ya Habari ilifanya mapitio ya mfumo wa leseni na udhibiti wa sekta ndogo ya utangazaji ili kuwezesha mazingira ya utendaji kazi katika sekta hiyo,” amesema
Uhuru wa habari
Pamoja na hayo Rais Samia amesema vyombo vya habari vipo huru kusema na kuandika wanayoyataka, muhimu kufuata mila na desturi zetu nchini, hilo ni muhimu sana, mila na desturi zetu nchini ni kuheshimiana, vyombo viheshimu na vyenyewe viheshimiwe.
“Uhuru maana yake ni kujiendesha wewe mwenyewe na kujiweza na kujitegemea, ndipo utakapokuwa huru, lakini kama unataka kuwa huru kusema, kesho unarudi Serikalini tubebe tusaidie, ili tuweze kusema, hapana uhuru hapo, sasa kama vyombo vya habari vinataka kuwa huru, viweze kujiendesha vyenyewe kama inavyojiendesha Azam,” amesema