NA NWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DODOMA
JUMLA ya vyeti 975 vimesajiliwa na WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA )kutokana na watu mbalimbali kuleta maombi yao ya kutaka kusajili cheti cha kuasili mtoto ambapo kwa mujibu wa sheria ya mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 imeweka utaratibu kuweza kusaidia watu wenye uhitaji.
RITA pia imetoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuasili mtoto kisheria ili kumuwezesha mtoto huyo kupata mahitaji yake ya msingi katika jamii yake.
Akizungumza katika maadhimisho ya wiki ya sheria yanayofanyika kitaifa mkoani Dodoma katika viwanja vya Nyerere Square, Ofisa Sheria kutoka RITA, Emmanuella Mwingira amesema kuwa, watu wengi hawafahamu umuhimu wa kufuata hatua za kisheria ili kuasili mtoto hivyo katika maadhimisho hayo RITA inatoa elimu hiyo kwa kina ili kuondoa sintofahamu hiyo katika jamii.
“Inafahamika kuwa katika jamii yetu ya kitanzania wapo watoto wanaokulia katika vituo vya kulelea watoto yatima ama kwasababu ya wazazi kufariki, hawajulikani walipo au hawana uwezo wa kuwapatia matunzo vivyohivyo wapo watu wazima ambao wanashauku ya kuwa na mtoto hata wa kuasili na hiyo ni kwasababu ya pengine kutojaaliwa kuwa na watoto wa kuwazaa lakini pamoja na hayo ni muhimu sana kufuata sheria ili kuasili mtoto rasmi” amesema. Emmanuella.
Emmanuella amesema jumla ya vyeti 975 vimesajiliwa na RITA kutokana na watu mbalimbali kuleta maombi yao ya kutaka kusajili cheti cha kuasili mtoto ambapo kwa mujibu wa sheria ya mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 imeweka utaratibu kuweza kusaidia watu wenye uhitaji.
“Kuasili mtoto kisheria ili kupata matunzo ya kudumu ya kifamilia ambapo suala hilo linasimamiwa na sheria ya kuasili Sura ya 335 toleo la mwaka 2002.“
“Hata hivyo Ili kuweza kusajili cheti cha kuasili mtoto kisheria katika ofisi za RITA muombaji anapaswa kuwasilisha nakala ya uamuzi kutoka mahakama kuu na pia cheti cha kuzaliwa cha mtoto anayeasiliwa ili kuwezesha mtoto kupata mahitaji yake ya msingi kama vile elimu, chakula, malazi na masuala ya afya kwa ujumla kama ambavyo watoto wengine wanapata katika jamii”
Ameongeza kuwa moja ya haki za mtoto ni kulindwa jambo ambalo watoto wasiokuwa na wazazi wamekuwa wakiteseka kwa kuishi mazingira ambayo si rafiki, hayana ulinzi na kupelekea kufanyiwa vitendo viovu na watu wasiokuwa na maadili kama vile kubakwa, kunyanyaswa kijinsia.
Amesema iwapo mtu atasajili cheti cha kuasili sheria itamchukulia kuwa ni sawa na mzazi halisi wa mtoto husika hivyo itasaidia pia kupunguza wimbi la watoto wa mitaani linalokuwa kila kukicha.
“Hii itasaidia pia kwa Serikali kuweza kupata takwimu sahihi ya wananchi wake katika kupanga mipango mbalimbali ya kimaendeleo katika jamii kama vile elimu,” amesema
Mbali na kutoa elimu ya kuasili katika maadhimisho hayo, RITA inatoa huduma ya msaada wa kisheria kuhusu usimamizi wa mirathi, kuandika na kuhifadhi wosia, elimu ya ufilisi,ndoa, talaka, usajili wa cheti cha kuzaliwa pamoja na maelezo ya kina kwa bodi za wadhamini wa taasisi kuhusu namna ya kuhuisha katiba zao.
Kazi nzuri
Asante pia tunaomba endelea kutembelea mtandao wetu kwa habari zaidi