NA MWANDISHI WETU, KILOLO
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametoa siku 10 kwa Waziri wa Maji, Juma Aweso kufika katika kata Uhambingeto iliyopo Wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa kushughulikia changamoto ya ukosefu wa maji iliyoripotiwa na diwani wa kata hiyo.
Chongolo amepewa malalamiko hayo alipofanya ziara yake leo Mei 31, 2023 katika kata hiyo huku baadhi ya wananchi wakiangua vilio na kuishutumu Kampuni ya Mshamindi Construction Ltd kuwa sababu ya wao kuendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.
Diwani wa kata hiyo, Tulinumtwa Mlangwa alisema wananchi wa kata yake walipata matarajio ya changamoto ya maji katika kata yao kushugulikiwa baada ya Julai mwaka jana kampuni hiyo kupewa tenda ya kufanya kazi hiyo.
Huku akilia kwa uchungu na kupiga magoti diwani huyo alimwambia Chongolo mradi huo wa thamani ya Sh bilioni 2.1 ulipaswa kukamilika Februari mwaka huu kabla mkandarasi huyo hajaongezewa miezi mingine minne inayoisha Juni, mwaka huu.
Pamoja na kuongezewa muda, diwani huyo alisema taarifa zinaonesha mkandarasi huyo amekwishalipwa malipo ya awali ya zaidi ya Sh bilioni 1.3 huku kazi iliyofanywa ikiwa ni asilimia 25 tu.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu hakuna kazi yoyote inayoendelea na matumaini ya wananchi wangu kupata huduma ya maji inayoyoma, sisemi haya ili nichaguliwe tena; nalia kama mwakilishi wao kwasababu najua changamoto hii ya maji inavyotutesa hususani wanawake,” alisema.
Hisia zake zikizua vilio toka kwa wananchi wengi, alisema wanalazimika kuendelea kutumia kwa pamoja na wanyama maji ya kwenye madimbwi kwa matumizi yao ya majumbani.