SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetumia Sh milioni 249.27 kununua mizani 82 ambayo itatumika kupima uzito wa mifugo wakati wa biashara katika minada ili kuifanya biashara hiyo kuwa na tija zaidi kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki aliyasema hayo katika hafla fupi ya kupokea mizani 82 iliyofanyika jijini Dar es Salaam Februari 6, 2023.
“Mizani inawekwa katika minada ili kuleta ushindani wa wazi wa bei kulingana na uzito wa mnyama, ni jukumu letu kuhakikisha mifugo tunayoiuza minadani inapimwa na tunajua uzito wake, ili tuweze kupata faida ya mifugo yetu,” amesema Ndaki
Amesema kwa muda mrefu biashara ya mifugon chini imekuwa ikifanyika kwa kukisia na kuangalia umbo la mfugo na si uzito halisi na hivyo kuifanya biashara kutokuwa na tija inayotarajiwa huku akibainisha kuwa lengo la Serikali ni kufunga mizani hiyo katika minada yote nchini lakini kwa kuanzia wameanza na hiyo 82.
“Jambo hili limekuwa halina tija kwa wafugaji kwa kuwa bei inayouzwa hailingani na uzito wa mnyama, hivyo huchangia kudhoofisha kipato cha wafugaji,”amefafanua
Alibainisha kuwa kwa kutambua changamoto hiyo na nyingine zinazoikabili Sekta ya Mifugo, Wizara iliamua kuja na mpango wa mabadiliko ili kuifanya sekta kutoka katika kufanya shughuli zake kienyeji na kuziboresha na kuwa za kibiashara.
“Mwaka huu wa fedha 2022/2023 tulitenga kiasi cha Shs.Milioni 249.27 kwa ajili ya kununua mizani 82 na tayari mizani hiyo yote imenunuliwa,” alibainisha
Aidha, amewataka wasimamizi wa minada kuhakikisha mifugo yote inayouzwa inapimwa na kumbukumbu za mifugo iliyouzwa na uzito wake zinawekwa.
“Pia hakikisheni mizani iliyonunuliwa na Serikali inatunzwa, endapo kutatokea uharibifu wa makusudi ili kuzuia zoezi hili la kupima mifugo, wahusika watawajibika,” alisisitiza
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Amani Mafuru amesema kwa muda mrefu mifugo iliyokuwa ikifika katika minada biashara imekuwa ikifanyika kwa makisio lakini Wizara ikaona umuhimu wa kuwepo kwa mizani hiyo.
“Hii itafanya biashara iwe ya uhakika hakuna mtu anayepunjwa, mfugo ukipimwa uuzwe kwa bei ambayo mfanyabiashara alitarajia na mnunuzi anunue kwa bei tarajiwa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akiongea na wafugaji, pamoja na wafanyabiasha wa mifugo ( hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya upokeaji na uzinduzi wa mizani za kupima uzito wa Mifugo ikiwa ni moja ya mpango wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Februari 06, 2023