Na Mohamed Saif
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso (Mb) ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuanza mara moja kuongeza mtandao wa usambazaji maji Kata ya Buswelu Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.
Ametoa maelekezo hayo Februari 4, 2023 alipofanya ziara kwenye tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita milioni 3 la Buswelu Mkoani Mwanza.
Akiwa katika mradi huo wa tenki, Waziri Aweso alielezwa kuwa licha ya tenki hilo kukamilika maeneo pekee yanayonufaika kwa sasa ni Buswelu, Bujingwa, Buhila, Buyombe na Mwashosha na kwamba bado kuna maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya maji.
“Haileti maana kuona tenki hili limekamilika lakini baadhi ya wananchi hawana huduma ya maji, dhamira ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan ni kumtua Mama ndoo kichwani na hapa bado Mama hajatuliwa ndoo kichwani,” amesisitiza Waziri Aweso.
Kufuatia maelezo hayo, Waziri Aweso aliiagiza Wizara ya Maji kuipatia MWAUWASA kiasi cha Sh milioni 500 ili kuhakikisha maeneo yanayopaswa kunufaika na tenki hilo yanafikishiwa miundombinu ya maji mara moja.
“Sisi Wizara hatutakuwa kikwazo kwa wananchi wa Buswelu kupata maji, MWAUWASA nataka kuona utekelezaji wa mradi huu unaanza mara moja ili kuwaondolea adha wananchi wa Buswelu,” ameelekeza Waziri Aweso.
Awali kabla ya ziara yake kwenye tenki hilo, Waziri Aweso alikutana na Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya MWAUWASA ambapo alielekeza masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma ya maji inaimarika kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake.
Aidha, mapema hivi leo Februari 6, 2023 ikiwa ni siku mbili tangu MWAUWASA kupokea maelekezo ya Waziri Aweso, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Meck Manyama ametembelea eneo hilo ili kujiridhisha na juu ya kuanza kwa utekelezaji wa maelekezo ya Waziri.
Akiwa katika eneo hilo, amekuta kazi za uchimbaji mitaro ya kulaza mabomba ya mtandao wa usambazaji maji zikiendelea kutekelezwa na baada ya kujiridhisha kuwa kazi inakwenda vizuri na kwa kasi Manyama ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maji hususan Mhe. Waziri Aweso kwa kuipatia MWAUWASA fedha haraka ili kuongeza mtandao wa usambazaji maji kutoka kwenye mradi wa tenki la maji Buswelu kwa kuhakikisha wananchi wa Kata ya Buswelu wanapata huduma ya majisafi na salama.
“Tumepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na tumeanza kuyatekeleza, ninaahidi kuwa maelekezo aliyotoa Waziri wetu wa Maji yanatekelezwa na kukamilika kwa wakati kwani tayari uchimbaji wa mitaro umeanza na baadhi ya bomba zimefika na ulazaji wake unafanyika, tunachimba na kulaza bomba vyote vinakwenda kwa pamoja,” amesema Manyama.
Manyama ametaja mitaa ya Kata ya Buswelu itakayonufaika kuwa ni Kadinda, Kigala, Buhila, Majengo na Halimashauri ambapo amesema zaidi ya wananchi 40,000 kutoka maeneo hayo watanufaika.
“Niwasihi wananchi wa maeneo ya mradi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu hii ambayo imeigharimu fedha nyingi Serikali yetu. Tunapenda kuona wananchi wanapata huduma endelevu,” amesema Manyama.