Na Mwandishi wetu
– Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Dk. Charles Msonde ameongoza kikao kazi kilichowakutanisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR – UTUMISHI), OR – TAMISEMI na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kilicholenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kiutumishi zinazowakabili walimu nchini.
Akifungua kikao hicho kilichofanyikia katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya TSC Makao Makuu Dodoma, Dk. Msonde amesema kuwa pamoja na kuwa Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha walimu wanapata maslahi yao, bado zipo changamoto kadhaa zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi ili walimu waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
“Serikali chini ya uongozi wa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan imefanya juhudi kubwa kuwasaidia walimu kupata maslahi yao. Kwa mfano, sasa hivi walimu wanaendelea kupandishwa vyeo kwa wakati, madai ya mapunjo ya mishahara na madai ya fedha za likizo yameelipwa kwa kiasi kikubwa na bado yanaendelea kulipwa. Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo bado tunaona zipo changamoto zinazowakabili walimu ambazo ni muhimu tuzitafutie ufumbuzi,” amesema Dk. Msonde.
Amesema kuwa ofisi hizo tatu (OR – TAMISEMI, OR – UTUMISHI na TSC) zimeamua kukutana pamoja kupitia changamoto moja moja na kuona na kuweka mikakati ya namna ya kuzitatua kwa kuwa ndizo zenye dhamana ya kushughulikia masuala ya walimu nchini.
“Waziri wetu, Mheshimiwa Angellah Kairuki amukuwa akifuatilia kwa karibu sana masuala ya walimu. Ametoa namba yake ya simu ili mwalimu yeyote mwenye changamoto aweze kuwasiliana nae moja kwa moja. Na kila siku anapokea simu za malalamiko ya walimu wetu na anatuagiza sisi wasaidizi wake kutafuta ufumbuzi wa malalamiko hayo. Hivyo, leo tunapaswa kuhakikisha tukitoka hapa masuala ya walimu yamekaa vizuri,” amesema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Dk. Msonde ameongeza kuwa ili kutatua changamoto hizo ni lazima kila mtendaji aliyepewa dhamana katika kusimamia walimu kuanzia ngazi ya shule, kata, halmashauri, mkoa na taifa kuhakikisha anakuwa msaada badala ya kuwa chanzo cha walimu kukosa haki zao.
“Tunafahamu kuwa zipo changamoto za kiutumishi ambazo zimesababishwa na masuala ya kimfumo, lakini zipo ambazo zinasababishwa na uzembe wa watendaji wetu. Ni muhimu tuelewe kwamba ili kuinua elimu Tanzania ni lazima sisi watendaji tuliopewa dhamana tuhakikishe tunawajibika katika nafasi zetu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,” amesema Dk. Msonde.
Kwa Upande wake, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama amepongeza jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuweka mazingira bora ya elimu na walimu nchini ambapo alieleza baadhi ya jitihada hizo kuwa ni walimu kuendelea kuajiriwa, kupandishwa vyeo, kubadilishiwa kazi waliojiendeleza kielimu, ujenzi wa nyumba za walimu na miundombinu mbalimbali ya shule.
“Tunampongeza Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye sekta yetu ya elimu, pia tunaipongeza OR – UTUMISHI kwa kazi nzuri waliyofanya kupandisha vyeo watumishi wa Umma wakiwemo walimu waliopandishwa vyeo wanathibitishwa na kulipwa mishahara kwa vyeo vyao vipya kwa wakati. OR – TAMISEMI tunawapongeza pia kwa namna wanavyofanya ufuatiliaji usiku na mchana kuhakikisha walimu wanakuwa na mazingira bora na wanatekeleza majukumu yao kikamilifu,” amepongeza Mwl. Nkwama.
Nkwama ametaja baadhi ya changamoto zinazosababisha malalamiko kwa walimu kuwa ni baadhi yao kukaa kwenye daraja/cheo kimoja kwa muda mrefu, kucheleweshwa kubadilishiwa cheo baada ya kujiendeleza kielimu, kutofautiana kwa vyeo kwa walimu wa kundi rika moja (walioanza kazi pamoja na wenye sifa sawa) pamoja na walimu wanaopanda vyeo pamoja kuidhinishiwa barua za kupanda vyeo kwa tarehe tofauti kwa sababu za kimfumo.