Na Mwandishi wetu
– Dodoma
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imekuwa miongoni mwa Taasisi chache za Serikali zilizotunukiwa cheti cha pongezi kwa kuandaa Mkataba wa Huduma kwa Mteja uliokidhi vigezo vinavyotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR – UTUMISHI).
TSC imeitunukiwa cheti hicho kilichoandaliwa na OR – UTUMISHI tarehe 23 Juni, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa mikataba ya huduma kwa mteja ya taasisi mbalimbali za Serikali ikiwa ni siku ya kilele cha wiki ya utumishi wa Umma.
Uzinduzi wa Mikataba hiyo ulifanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejeimenti ya Utumishi wa Umma na Utala Bora, Mhe. George Simbachawene katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ambapo cheti cha TSC kilipokelewa na Katibu wa Tume hiyo Mwl. Paulina Nkwama.
Katika hotuba yake, Waziri Simbachawene amezipongeza taasisi zilizoandaa mikataba hiyo kwa kuzingatia vigezo vilivyotolewa na kusisitiza kuwa yote yaliyoelezwa katika mikataba hiyo yazingatiwe ili wananchi waweze kupata huduma bila usumbufu.
Akifafanua Mkataba wa Huduma kwa Mteja, Waziri Simbachawene amesema unakusudia kuwawezesha wateja (wananchi) kuelewa majukumu ya taasisi husika, huduma zinazotolewa, haki na wajibu katika kupata huduma, taratibu za kupata huduma na hivyo kuimarisha uhusiano kati ya taasisi na wateja wake.
“Mkataba wa huduma kwa mteja ni muhimu sana kwani unasaidia Serikali kutoa huduma bora na hivyo wananchi kuifurahia na kuipenda Serikali yao kwa kuwa inawaletea maendeleo. Ninazielekeza Taasisi zote za Serikali ambazo bado hazina Mkataba wa Huduma kwa mteja kuhakikisha zinaandaa mkataba huo mara moja kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Ofisi yangu,” amesema Waziri Simbachawene.
Aidha, Waziri amewasisitiza Taasisi zote za Serikali kuhakikisha Mikataba hiyo inatekelezwa kikamilifu na kuondoa urasimu katika utoaji wa huduma unaosababisha usumbufu na wakati mwingine wananchi kukosa huduma.
“Lazima tuelewe kuwa kwa kila tunachokifanya lengo letu ni kumsaidia mwamanchi kupata huduma kwa urahisi. Kuna baadhi ya watendaji imekuwa ni kawaida yao kuleta urasimu na usumbufu kwa wananchi kwa kisingizio cha kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu bila kuangalia wajibu wake katika kuhakikisha mwananchi anapata huduma.”
“Kama huduma yako ni kuwapatia wanachi maji tuhakikishe maji yanapatikakana. Wapo baadhi ya watumishi kazi yao ni kusema tunafuata kanuni na taratibu, mwanachi anakuja ofisini wewe kazi yako ni kumwambia hujafuata taratibu siwezi kukuhudumia, hiyo siyo sawa. Kanuni na taratibu zipo lakini mwananchi anachotaka ni kupata huduma na wakati mwingine hizo kanuni na taratibu wala hazijui. Ni lazima tuangalie zaidi matokeo ya maamuzi yetu kama yanamsaidia mwananchi au yanamwongezea maumivu,” amesema Waziri Simbachawene.
Sambamba na hilo, Waziri huyo ameagiza watumishi wote wa umma kuvaa beji zenye majina yao muda wote wakiwa kazini ili kusaidia wanachi kuwatambua na pale inapotokea mwananchi hakuridhishwa na huduma iwe rahisi kwa mtumishi husika kubainika.
Pia, amewasisitiza Watumishi wa Umma kuepuka mazingira yanayochochoa rushwa katika kutoa huduma kwani kufanya hivyo kunasababisha wananchi kukosa haki zao na hivyo kuichukia Serikali.
“Ni Lazima tuzingatie Miiko na Maadili ya Utumishi wa Umma, tuwahudumie wananchi kwa usawa. Usijaribu kumpendelea mtu na kumkandamiza mwingine, tuepuke kujihusisha na rushwa kwa namna yoyote ile. Tuelewe kwamba mwananchi asiporidhika na huduma unayompa hakuangalii wewe tu bali anaona Serikali yote ndio iko hivyo na anaanza kuichukia,” amesema Waziri.
Pamoja na hayo, amewataka watendaji (viongozi) wenye tabia ya uonevu na unyanyasaji kwa watumishi walio chini yao kuacha tabia hiyo maramoja kwani ni kinyume na maadili na inasababisha msongo kwa watumishi na kudorora kwa utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Ninajua huko kwenye taasisi zetu zipo shida, unakuta kiongozi hampendi tu mtuishi wake, sasa utakuta mtumishi huyo anafanyiwa visa, wakati mwingine anasingiziwa kesi ilimradi tu afukuzwe kazi. Unakuta mtumishi anatoka nyumbani kwake lakini badala ya kufurahia kazi na kuwa tayari kuwahudumia wananchi anaanza kuwaza sijui leo kiongozi wangu atakuja na lipi, sasa kwa utaratibu huo mkataba huu utakuwa hauna maana,” amesema.
Waziri huyo ameahidi kufanya ziara na kufanya mikutano na watumishi wa Umma ili kusikiliza kero na changamoto wanazokutana nazo wakiwa kazini ili kuona namna bora ya kuzitatua.