NA MWANDISHI WETU
KAMPENI ya kuhamasisha matumizi ya Mastercard na QR Code ‘Lipa Mkononi’ iitwayo NMB MastaBata ‘Kote Kote’, imefikia ukomo Jumanne Februari 7, kwa wateja 7 na wenza wao kujishindia safari ya Dubai kwa siku nne inayogharamiwa kila kitu na Benki ya NMB, kuhitimisha miezi mitatu iliyotoa zawadi mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 350.
NMB MastaBata ‘Kote Kote’ ni msimu wa nne wa kampeni hiyo uliozinduliwa Oktoba 28 mwaka jana, ikichagiza matumizi yasiyohusisha pesa taslimu ‘cashless,’ ambako kulikuwa na zawadi za kila wiki, mwezi na ‘grand finale’ hiyo iliyohusisha pia wafanyakazi wawili wa benki hiyo kinara nchini.
Katika droo ya fainali iliyosimamiwa na Pendo Mfuru kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), walioibuka washindi wa safari ya Dubai ni: Upendo Yohana Msanjila (Dar), Edwin Sett Mwakabage (Kilimanjaro) na Benigna Xaveria Hyera (Dar).
Washindi wengine wa droo hiyo iliyochezeshwa na Balozi wa NMB MastaBata ‘Kote Kote’, Millard Ayo, ni pamoja na Nazia Abdulsatar Lakha (Dar), John Wayne Lubisha (Dodoma) na Chintan Chandrakant Kamania (Dar).
Kabla ya ‘grand finale’ hiyo, jumla ya washindi 750 walishinda pesa kiasi cha Sh. 100,000 kila mmoja, wengine 98 wakizawadiwa Sh. Mil. 1 kila mmoja, huku washindi 12 wakitwaa bodaboda moja moja zenye thamani ya Sh. Mil. 3 kila moja. Aisha, washindi wengine wanne walijishindia safari ya Zanzibar kuhudhuria Tamasha la NMB Full Moon Party.
Awali, kabla ya droo ya fainali, Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, alibainisha kuwa kampeni hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa kwa kufanikiwa kubadili tamaduni za matumizi ya kadi na QR Code, na kuwa matokeo ya faida kubwa ya Sh. Bilioni 429 baada ya kodi kwa mwaka 2022, yametokana na promosheni kama hizo.
“Ni kampeni chanya iliyoongeza matumizi ya kadi, ambayo ni salama, rahisi na nafuu zaidi, huku ikitoa mchango katika rekodi yetu ya faida baada ya kodi. Wito wetu Kwa Watanzania, wafungue akaunti na kufanya matumizi yasiyohusisha pesa taslimu, ili kujiweka katika nafasi za kunufaika na kampeni zaidi zijazo na promosheni nyinginezo,” alibainisha Mponzi.
Mapema kabla ya droo hiyo, Philbert Casmir ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Kadi NMB, alisema benki yake inajivunia mafanikio yaliyotokana na MastaBata ‘Kote Kote’, kampeni endelevu iliyokuwa na malengo matatu ya kuzawadia washindi, kuhamasisha matumizi salama na nafuu ya kadi, pamoja na kurejesha kwa Jamii sehemu ya faida yao kwa mwaka uliopita.
Naye Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Pendo Mfuru, aliipongeza NMB kwa aina ya ushirikiano iliyonao kwa taasisi yake iliyo na mamlaka ya kusimamia michezo hiyo nchini, ikiwamo kuratibu, kuendesha na kuzawadia washindi kwa kuzingatia vigezo na masharti ya GBT, huku akiwapongeza zaidi ya washindi 870 walioibuka na zawadi mbalimbali za kampeni hiyo.