NA MWANDISHI WETU
-Njombe
MKUU wa wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Victoria Mwanziva ametoa wito kwa vijana wilayani humo kutumia mashindano ya michezo yanayofanyika wilayani humo kukuza na kutangaza vipaji vyao ili waweze kuzifikia ndoto zao.
Amebainisha hayo wakati akizungumza na kamati ya maandalizi ya mashindano ya mpira wa miguu ya Kuambiana Cup yanayotarajiwa kuzinduliwa Julai 15 mwaka huu wilayani humo huku viongozi mbali mbali akiwemo mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka pamoja na Naibu Waziri wa Sanaa,Utamaduni na Michezo Hamis Mwinjuma (MWANA FA) wakitarajiwa kushiriki.
“Vijana waitokeze ili waweze kuweka wazi vipaji vyao kwasababu kushiriki mashindano kama haya ni kujiongezea wigo na kuweza kupanda juu zaidi na kimsingi mashindano kama haya yanchagiza sana ukuaji wa soka kwenye wilaya yetu”amesema DC Mwanziva
Mratibu wa mashindano hayo John Kiparamoto amesema mashindano hayo yamefikia msimu wa nne tangu yalipoanzishwa ambapo kwa msimu huu wameongeza wigo wa ushiriki wa kuongeza tarafa ya Mawengi ambapo pia Bondia maarufu Karim Madonga akitarajiwa kushiriki na kuwaomba mabondia wilayani humo watakaopenda mchuano wa ngumi kujitokeza.