NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha kuwa mikataba ya utekelezaji wa makubaliano ya uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World itazingatia maslahi ya nchi na kuleta manufaa kwa Taifa letu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 28, 2023) wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo amesisitiza kuwa makubaliano yaliyoingiwa yanalenga kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa kuwa bandari ya Dar es salaam ndiyo kitovu cha huduma za bandari nchini Serikali iliamua kutafuta Kampuni yenye uwezo na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa bandari duniani kwa teknolojia za kisasa ili kuiwezesha bandari hiyo kufanya kazi kwa ufanisi, kuongeza mapato ya nchi na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi.
Amesema Serikali za Tanzania na Dubai zimeingia makubaliano kwa lengo la kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na wa kijamii katika uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini kupitia Kampuni ya DP World, ambayo imeonesha kuwa na utaalamu, uwezo na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa bandari 190 katika nchi 68 barani Afrika, Asia, Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Kusini.
“Kuhusu umiliki wa bandari, nilihakikishie bunge lako na wananchi kwa ujumla kwamba, kupitia Sheria ya Bandari ya Mwaka, 2004, Mamlaka ya Bandari Tanzania imekasimiwa haki ya kuwa mmiliki wa maeneo yote ya bandari nchini na haina uwezo wa kutoa umiliki huo kwa kampuni nyingine. Haki iliyopewa kwa mujibu wa sheria hiyo ni kuingia mikataba ya ushirikiano wa kupangisha na kuruhusu sekta binafsi kuendesha sehemu ya maeneo hayo.”
Waziri Mkuu amesema wakati wote wa utekelezaji wa makubaliano hayo na mikataba itakayoingiwa, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kutekeleza majukumu yao katika eneo la mradi kama vilivyofanya katika kipindi cha miaka yote 22 ya mkataba na mwekezaji wa awali (TICTS) aliyemaliza mkataba wake. “Kuhusu mapato, ninapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaendelea kusimamia masuala ya mapato ya Serikali kutoka kwa mwekezaji kwa mujibu wa sheria na mkataba.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kupokea mapendekezo, maoni na ushauri kutoka kwa waheshimiwa wabunge, wananchi na wadau mbalimbali. “Kwa msingi huo, niielekeze Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iendelee kuratibu utoaji wa elimu na ufafanuzi wa hoja za wananchi.
“Nitumie fursa kutoa rai kwa Watanzania wenzangu tusiruhusu mgawanyiko wa aina yoyote ile tunapotoa maoni yetu kuhusu uwekezaji wa bandari, tuepuke kujadili itikadi za kisasa, udini, ukabila, ukanda au vyovyote vile, muhimu tuenzi tunu yetu ya amani na mshikamano wa Taifa letu iliyojengwa na waasisi wetu.”
Amesema Juni 10, 2023 Bunge lilipata fursa ya kuchangia, kuishauri Serikali na kupitisha azimio la mapendekezo ya kuridhia makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini, hivyo amewapongeza wabunge wote kwa michango yao na kwa kuona umuhimu na tija katika jambo hilo na kuamua kulipitisha azimio hilo.