Na Mwandishi Wetu Mbeya.
Maonesho makubwa ya Siku ya wakulima Nane nane yanayotarajiwa kuzikutanisha zaidi ya nchi 30 Jijini Mbeya yamepewa sapoti kubwa na Benki ya NMB kwa kudhamini jumla ya Shilingi Milioni 80.
Akikabidhi mfano wa Hundi kwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya Kaimu Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Frank Rutakwa amesema kwa kipindi cha miaka sita cha maonesho hayo ambayo yamekuwa yakifanyika Kitaifa mkoani Mbeya,Benki hiyo imedhamini jumla ya Shilingi Milioni 255.
Amesema NMB imekuwa ikithamini mchango wa wakulima katika kukuza uchumi wa Taifa hivyo wao kama wadau wameona ni vyema kushirikiana na serikali katika kufanikisha maonesho hayo ya wakulima.
“Kusaidia sekta ya kilimo ni fahari yetu,kupitia kilimo Benki yetu imekuwa ikifanya biashara kubwa inayochangia ukuaji wa sekta ya kilimo Nchini” alisema Rutakwa.
Ameongeza kuwa kwa kuthamini mchango wa kilimo katika ukuaji wa uchumi, NMB imeweka idara maalumu ya Kilimo na Mameneja uhusiano kwenye kila kanda ili kuhakikisha kilimo kinafanikiwa na kinakuwa msingi imara kwa uchumi wa nchi yetu.
Akizungumza mara baada ya kupokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 80 kutoka Benki ya NMB,Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera alionyesha shukrani kubwa kwa msaada na ukaribu wa Benki ya NMB katika kusaidia sekta ya kilimo.
Mkuu huyo wa Mkoa ambae pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maonesho ya Nane Nane alisema NMB imezidi kuonesha ukomavu wake kwa kuendelea kutoa udhamini mkubwa kwenye maonesho ya siku kuu za Wakulima ya Nane nane Kanda Nyanda za juu zinazofanyika kwa mfululizo Kitaifa mkoani Mbeya.
“Benki ya NMB ni mojawapo ya taasisi za kifedha zinazoongoza nchini Tanzania kwa kuchangia kwa dhati juhudi za serikali katika kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi na sekta zingine hususani za Elimu na Afya ambazo wamekuwa mstari wa mbele kutoa michango mara kwa mara,” Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, alisema mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini inayojumuisha mikoa saba inajivunia uwepo wa Benki ya NMB kutokana na mchango wake kwa wakulima na serikali.
Homera amesema mbali na mchango wa fedha wa kwa maonesho ya Wakulima Benki hiyo imekuwa ikitoa elimu na semina kwa vikundi vya wakulima wanaoshiriki maonesho ya Nanenane na hivyo kufanya maonesho hayo kuwa ni sehemu ya shamba darasa.
“Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa jitihada zenu za kusaidia kukuza uchumi kupitia kilimo,tutaendelea kuwashawishi wananchi waendelee kujitokeza kufungua akaunti kwenye Benki hiyo, mrejesho wake umekuwa ni chanya kwetu”amesema RC Homera.
Kupitia mipango mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa wakulima, upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo, na suluhisho za kidijitali zilizoundwa mahsusi kwa ajili ya jamii za vijijini, benki ya NMB imejijengea sifa nzuri kama mshirika imara katika sekta ya kilimo.
Maonesho ya Nanenane yanayokaribia yanatarajiwa kuleta matumaini makubwa kwa wadau na washiriki, ambapo kutakuwa na maonyesho mbalimbali ya kilimo, maonesho ya vitendo, na vikao cha kubadilishana ujuzi. Tukio hili linaahidi kuwa sherehe yenye uhai inayoonyesha uwezo mkubwa wa kilimo nchini Tanzania, na udhamini wa benki ya NMB unathibitisha dhamira yao isiyoyumba katika kukuza maendeleo ya nchi.
Kwa ushiriki huu kutoka benki ya NMB na wadhamini wengine, maonesho ya Nanenane yanatarajiwa kukuza ubunifu katika kilimo, kuhamasisha uwekezaji, na kuchochea maendeleo endelevu katika Mkoa wa Mbeya na maeneo mengineyo.