Jarida la Kimataifa la Euromoney laitaja NMB kuwa Benki Bora na Benki Bora ya Wateja Maalum 2023
NA MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
JULAI 12, mwaka 2023, Benki ya NMB ilitunukiwa tuzo tatu kutoka kwenye majarida yam masuala ya kibenki ya kimataifa yaliyoitaja kuwa Benki Bora Tanzania 2023, Benki Bora ya Wateja Maalum (Best Private Bank) na Benki Bora ya Wateja Binafsi nchini 2023.
Kwa mara ya kumi ndani ya miaka 11, NMB imetajwa kuwa Benki Bora Tanzania kwenye Tuzo za Ubora za Euromoney 2023 ambapo pia ilitunukiwa ushindi wa Benki Bora ya Wateja Maalum 2023 kwa mara ya kwanza. Benki pia imetambuliwa kama Benki Bora ya Wateja Binafsi nchini na Jarida la kimataifa la Global Banking and Finance Review. Hizi zote ni tuzo za kimataifa zinazotolewa na majarida yanayo angalia masoko ya fedha yaliyoko jijini London.
Tuzo ya Benki Bora ya Euromoney Tuzo ya umahiri ya Euromoney imeitambua benki ya NMB kwa ufanisi wa kiutendaji kwa ujumla, mkakati wa matumizi ya njia za kidijitali, huduma jumuishi za fedha na ufanisi wa hali ya juu, uwezo wa benki ya NMB kuwekeza zaidi kwenye biashara inayomlenga kila Mtanzania. Jopo la majaji wabobevu wa tuzo za Euromoney pia walizingatia hadhi ya benki kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi endelevu nchini.
Tuzo ya Benki Bora ya Wateja Binafsi Tanzania ilitambua mchango mkubwa wa benki katika kuwajumuisha wananchi kwenye mifumo rasmi ya kifedha kupitia uwekezaji wa kidijitali, bidhaa na suluhisho zinazozingatia mahitaji ya walio wengi na kutoa mwelekeo wa kimkakati kuyafikia makundi ambayo hayajahudumiwa kikamilifu. Jopo la majaji wa tuzo zote mbili waliuona ubora na nguvu ya biashara ya kuwahudumia wateja binafsi kama mfano mzuri wa lengo la taasisi inayofanya kazi kwa weledi.
Akizungumzia tuzo hizo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB – Ruth Zaipuna -alisema: “Uwekezaji makini tunaoendelea kufanya kwenye teknolojia na kiutawala unaleta matokeo chanya kwa kuibadilisha NMB si tu kama benki kiongozi nchini, lakini pia kama taasisi inayozidi kusifika kikanda na kimataifa kwa ubora wa huduma za kibenki, ubunifu na suluhisho zinazoleta mabadiliko.”
Bi Zaipuna aliongeza kuwa ushindi wa tuzo ya Benki Bora, Benki Bora ya Wateja Maalum na Benki Bora ya Wateja Binafsi 2023 ni kielelezo tosha kuwa jitihada zetu zinatambulika si tu Tanzania bali pia nje ya nchi. “Tuzo hizi ni mafanikio ya kutia moyo kwetu, wateja wetu, na washirika wetu,” alisema Bi Zaipuna.
Akikabidhi tuzo ya Benki Bora Tanzania, mhariri wa Jarida la Euromoney, Louise Bowman, alisema: “Mwaka 2022 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa kwa NMB. Kipindi cha matokeo ya kifedha na yasiyo ya kifedha yaliyovunja rekodi kulipelekea kupatikana kwa thamani kubwa kwa wanahisa na mapato thabiti. Ubora wa mkakati na uwekezaji wa benki ulibainika kupitia matokeo muhimu ambayo ni pamoja na ukuaji wa akaunti za wateja, upatikanaji thabiti na endelevu wa mapato, na kuongezeka kwa shughuli za wateja hasa kwenye mifumo ya kidijitali.”
Kuhusu Tuzo za Ubora za Euromoney
Tuzo za kila mwaka za Ubora za Euromoney hutambua benki zenye uwezo wa kutumia vitengo vyake mbalimbali kukidhi mahitaji ya wateja wao. Tuzo hizo pia utambua benki zinazoendana na mazingira ya soko na matakwa ya kiudhibiti na ambazo ni za viwango vya kimataifa kwa jinsi zinavyoendeshwa na kutoa huduma.