Urusi inasema miili 10 na vinasa sauti vimepatikana katika eneo la ajali ya ndege inayodhaniwa kumuua chifu wa Wagner Yevgeny Prigozhin.
“Majaribio ya kijenetiki ya molekuli sasa yanafanywa,” wachunguzi wanasema.
Ndege hiyo ilianguka karibu na Moscow siku ya Jumatano, na kusababisha uvumi kwamba bomu au kombora ndilo la kulaumiwa.
Madai kwamba Kremlin ilitoa amri ya kuua Prigozhin ni “uongo mtupu”, msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin aliambia BBC mapema.
Prigozhin – ambaye wakati mmoja alikuwa mwandani wa Putin – aliongoza uasi wa silaha dhidi ya Urusi akiwaongoza wapiganaji wa Wagner mwezi Juni.
Bw Putin wakati huo alielezea uasi huo kama “uhaini”, lakini makubaliano yaliafikiwa kwa mamluki wa Wagner kujiunga na jeshi la kawaida la Urusi au kwenda Belarus – mshirika wa Moscow.
Hata hivyo, kutokana na uasi huo, waangalizi wengi walimtaja Prigozhin, 62, kama “mtu anayetembea akiwa amekufa “, wakisema kuwa rais wa Urusi hatawahi kumsamehe mkuu huyo wa Wagner.
Wakati wa mkutano wa Ijumaa na waandishi wa habari, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliiambia BBC kwamba kulikuwa na “uvumi mwingi” kuhusu vifo vya “kutisha” vya watu wote 10 katika ajali ya ndege ya Jumatano katika eneo la Tver, kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Urusi.