Na Ashrack Miraji
-BEST MEDIA, KILIMANJARO
MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuhamisha gulio linalofanyika Jumatano hadi Jumapili eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanja vya michezo maarufu Kwasa-kwasa na kusababisha malalamiko kwa wanamichezo ambao wanashindwa kutumia eneo hilo.
Pamoja na hilo, ameonyesha kutoridhishwa na hali ya Soko Kuu la Mji wa Same kutokana na uchafu uliokithiri huku vyoo vinavyotumika kukosa ubora hali inayosababisha kuhatarisha usalama wa afya kwa wafanyabiashara na wanunuzi wanaotumia soko hilo.
Kutokana na hali hiyo ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same, kukarabati vyoo vinavyotumika sokoni hapo kufikia Septemba ya mwaka huu 2023.
Agizo hilo amelitoa alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa soko hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Wilaya ya Same ambapo amesisitiza uboreshwaji wa miundombinu na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.
Awali wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mji wa Same, wakitoa malalamiko yao wamemweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa soko hilo linakabiliwa na ubovu mkubwa wa miundombinu, uwepo wa mashimo makubwa yaliyo ndani ya soko pia kukosekana nishati ya umeme hali inayosababisha kuendesha biashara kwa shida wakitaharisha pia usalama wao.