(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikali WFM – DSM)
Na Josephine Majura, WF, Dar es Salaam
SERIKALI imewaalika wadau wa Sekta Binafsi kutoka Uingereza kuwekeza nchini ili kusaidia juhudi za Serikali kufikia malengo yake.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna wa Biashara wa Ukanda wa Afrika wa Serikali ya Uingereza, John Humphrey.
Chande amesema Serikali imekamilisha utiaji saini na UK Export Finance kwenye Mradi wa Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na kuendeleza Barabara ya Tunguu – Makunduchi yanye urefu wa kilomita 28, Fumba – Kisauni-Mazizini – kilomita 13.2, na mkoani – Chake Chake and Pemba Airport kwa urefu wa kilomita 43.5
Katika kikao hicho Naibu Waziri wa Fedha, Chande amewakaribisha wawekezaji mbalimbali kutoka Uingereza kuja kuwekeza katika sekta za uzalishaji, uongezaji thamani na utalii nchini Tanzania.
“Nakukaribisha wewe na wafanyabiashara na wawekezaji wa kiingereza kuleta mitaji yenu Tanzania,” amesema Chande.
Kwa upande wake Kamishna wa Biashara wa Ukanda wa Afrika wa Serikali ya Uingereza, John Humphrey , amesema watashirikiana na Serikali kufanya kazi pamoja na kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika na kuendekeza kuwekeza katika vipaumbele vya kibiashara vilivyopo nchini Tanzania.