Apongeza kazi kubwa iliyofanyika, awasisitiza wataalamu kukamilisha mradi kwa wakati
Na Zuena Msuya, Pwani,
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka, amesema kuwa watanzania wanahitaji kupata huduma ya umeme wa uhakika na kwamba ameridhishwa na kazi kubwa ya utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).
Balozi Kusiluka ameeleza hayo tarehe 6 Septemba, 2023 wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa JNHPP ili kuona maendeleo ya Mradi huo unaotarajiwa kuzalisha Megawati 2115 za Umeme ambao unatekelezwa katika Mkoa wa Pwani.
Amewasisitiza wataalamu wanaotekeleza mradi huo kuwa wahakikishe kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati kwani watanzania wanausubiri kwa hamu kubwa na wanataka kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali yao.
“Najua kazi kubwa imefanyika nimeamua kuja kuona ili kuamini. Kwa ujumla kazi ni nzuri sana imefanyika, ujenzi umefika zaidi ya asilimia 90, Serikali imewekeza fedha nyingi hivyo napenda kuwaambia watu wote na watanzania kwa jumla watarajie kupata umeme wa uhakika muda si mrefu baada ya mradi kukamilika”, alisema Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Kusiluka.
Napenda kumshukuru na kumpongeza Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza ujenzi wa mradi huo kwani alipoingia maradakani ujenzi wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 35, na sasa ni miaka miwili na nusu tangu ameingia madarakani mradi huo umefikia zaidi ya asilimia ya 90 na unatarajia kuzinduliwa mwakani.
Aidha niwapongeze wahusika wote waanaotekeleza mradi huo kwa kuanza na Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme nchini (TANESCO), na wadau wengine, ni fahari kubwa kuona mradi mkubwa kama huo umetekelezwa na watanzania kwa kuhusishwa na kushirikishwa kwa kiasi kikubwa sana kuanzia mwanzo hadi sasa.
Ni matumaini yetu kwamba mpaka sasa vijana na wataalamu wetu wameweza kujifunza mambo mengi sana, na mara tu baada ya mkandarasi kuondoka, tunaamini watanzania hao watakuwa wamepata utaalamu na ujuzi mkubwa zaidi wa kuendesha kituo cha JNHPP na kutekeleza miradi mingine ya kuzalisha umeme kama huu.
Ameieleza timu ya wataalam wanaotekeleza mradi huo kuwa walianza vizuri mradi huo na wamalize vizuri na kwa wakati huku wakitambua kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi na watanzania wanausubiri kwa hamu na wanataka kunufaika na matunda ya uwekezaji huo mkubwa na muhimu kwa Taifa letu.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Kiongozi aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Faraji Kasidi Mnyepe, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande na viongozi wengine kutoka Wizarani, JWTZ na TANESCO.