Na Veronica Simba – REA
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeahidi kugharamia gharama zote za kuunganisha umeme katika Shule ya Msingi ya Chifu Hangaya wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, inayojengwa kwa ufadhili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ikumbukwe Rais Samia alisimikwa kuwa Chifu Mkuu wa Machifu Tanzania wakati wa Hafla iliyofanyika Agosti 8, 2021 katika Viwanja vya Red Cross eneo la Kisesa, wilayani Magu na kupewa jina la Chifu Hangaya hivyo shule hiyo imepewa jina lake.
Ahadi hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, Rachel Kassanda, akiwa ameongoza Ujumbe wa Bodi katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini wilayani humo.
Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi aliofuatana nao, ambao ni Mhandisi Styden Rwebangila na Florian Haule, Mwenyekiti alisema REA inaunga mkono jitihada za Rais Samia za kuwaletea wananchi maendeleo hivyo itafadhili uunganishaji umeme ili ndoto yake njema kuona watoto wote wanapata elimu bora itimie.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya aliishukuru REA kwa ahadi hiyo akisema kuwa nishati ya umeme itawezesha shule hiyo iliyo katika hatua za mwisho kukamilika kutoa elimu bora kwa watoto.
Katika hatua nyingine, Bodi imeahidi kuzisaidia kaya maskini zaidi, hususan zile zilizoko katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), ambazo zimefikiwa na miradi ya umeme vijijini, kwa kuzipatia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) bure ili kuwawezesha wakazi wake kuepuka gharama za kutandaza nyaya katika nyumba zao.
Aidha, Bodi imetoa hamasa kwa Maafisa Uchumi na Mipango wa Wilaya kote nchini, kuainisha fursa zilizoko katika maeneo yao kwa wananchi ambao wamefikiwa na miradi ya umeme vijijini ili waitumie nishati hiyo kuchangamkia fursa hizo kwa ajili ya kuinua hali yao kiuchumi.
Awali, Ujumbe wa Bodi ulifanya ziara katika Wilaya ya Ilemela ambapo ulikutana na Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Masala pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali.
Bodi imeahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazohusu umeme vijijini zilizowasilishwa na viongozi hao wa Wilaya za Ilemela na Magu ili kuhakikisha azma ya Serikali kuwapatia wananchi maendeleo kupitia nishati hiyo inafikiwa kikamilifu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoani Mwanza, Mhandisi Ernest Makale, jumla ya miradi sita ya umeme vijijini inatekelezwa katika Mkoa huo ambapo ikikamilika itakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi.
Bodi ya Nishati Vijijini inaendelea na ziara katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini ambapo katika hatua za awali, imeeleza kuridhishwa na kasi ya Wakandarasi inayoleta matumaini kuwa itakamilika kwa wakati.