Na MWANDISHI MAALUMU
-SAUDI ARABIA
Ujumbe wa Tanzania unaohudhuria Mkutano wa 45 wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO unaoendelea Riyadh, Saudi Arabia, umeendelea kutetea kwa hoja maeneo yake kubaki kwenye orodha ya Urithi wa Dunia na kuahidi kuendelea kuyalinda maeneo hayo kwa gharama zozote ikiwa ni dhamira endelevu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Maeneo ya Tanzania ambayo taarifa zake mpaka sasa zimewasilishwa katika Kamati hiyo ni pamoja na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba Selous, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara na Mji Mkongwe wa Zanzibar ambapo Waziri wa Utalii na Malikale Zanzibar, Simai Mohammed Said kwa upande wake leo alieleza jinsi uhifadhi wa Mji huo muhimu kiutalii unavyopewa kipaumbele chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza katikati mwa Mkutano huo Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, ameeleza pamoja na Tanzania kuwasilisha ripoti zake na kujadiliwa au kupitishwa bila kujadiliwa, Mkutano huu pia ni wa kujifunza kutoka nchi nyingine.
“Maeneo mengi ya Urithi wa Dunia yanafanana hivyo moja ya mafanikio ya Mkutano huu ni fursa ya kujifunza changamoto na mafanikio kutoka mabara na nchi nyingine katika uhifadhi wa maeneo hayo na raslimali zilizomo,” alisema Dk. Abbasi.