Home KITAIFA KAMPUNI YA QWIHAYA YATOA MSAADA ILEMELA

KAMPUNI YA QWIHAYA YATOA MSAADA ILEMELA

Google search engine

NA DENIS MLOWE 

Kampuni ya Qwihaya General Enterprises LTD ya mjini Mafinga Mkoani Iringa imetoa msaada wa  vipande vya mbao 

2,200 vya kupaulia kwa ajili ya kujenga upya makazi yao.

Msaada huo umetolewa ikiwa na Lengo la kurejesha tabasamu miongoni mwa wakazi zaidi ya 350 kutoka kaya 50 za mitaa ya Buganda na Ilemela Mahakamani Manispaa ya Ilemela ambao nyumba zao zilibomolewa kwa mvua iliyoambatana na upepo mkali.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh13.2 milioni umekabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Qwihaya, Benedicto Mahenda Qwihaya ikiwa ni kuitikia wito wa Serikali kwa wadau kujitokeza kusaidia waathirika kujenga upya makazi yao baada ya janga hilo lililotokea Septemba 6, mwaka huu.

Kupitia msaada huo, kaya 16 za Mtaa wa Buganda ambao nyumba zao zilibomoka kabisa zimepata vipande 47 vya mbao huku kaya nyingine 13 ambazo nyumba zao hazikupata madhara makubwa zikipewa mbao 30 kila moja.

Msaada kama huo pia umetolewa kwa Kaya 21 kutoka Mtaa wa Ilemela Mahakamani ambao pia waliathiriwa na mvua hizo zilizowaacha wananchi wakilala nje kwa kukosa makazi.

Akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Qwihaya, Benedicto Mahenda amesema uongozi wa kampuni hiyo inayojihusisha na biashara ya mazao ya misitu uliguswa na taarifa za janga hilo zilizotangazwa kupitia vyombo vya habari ikiwaonyesha watoto, wazee na wanawake wakiwa wamelala nje kwa kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.

“Tumetoa sehemu kidogo ya tulichojaaliwa na Mwenyezi Mungu kusaidia waathirika kujenga upya makazi yao,’’ amesema Mahenda

Akishukuru kwa niaba ya wenzake, Regina Chrisant, mmoja wa waathirika, mkazi wa Mtaa wa Buganda ameishukuru kampuni ya Qwihaya, Serikali na wadau wote kwa misaada inayowawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida baada ya janga lililowaacha wakiwa hawana makazi.

‘’Misaada hii ya hali na mali imeturejeshea matumaini siyo kwa kwa kutuwezesha kuyajenga upya makazi yetu, bali pia inaonyesha jinsi Watanzania tunavyoishi kwa upendo miongoni mwetu,’’ amesema Regina

Stanslaus Francis, mwathirika mwingine aliyepokea msaada ameomba wadau zaidi kujitokeza kusaidia waathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida baada ya janga hilo ambalo alikusababisha majeruhi wala vifo.

Shukrani zingine zimetolewa na Diwani wa Kata za Shibula iliko Mtaa wa Buganda, Swila Dede (CCM) huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza kuitikia wito wa Serikali wa kusaidia wananchi kwa sababu bado kuna mahitaji mengi ikiwemo ya chakula, samani za ndani na vifaa vingine vya ujenzi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buganda, Evarsit Chikanga amewataka wanaopokea msaada kuitumia kwa malengo mahusui ikiwemo kujenga upya makazi yao huku Mratibu wa Maafa Manispaa ya Ilemela, Jamses Wembe akiwataka wananchi wanaoishi jirani na fukwe na wanaofanya shughuli za kiuchumi na kijamii ndani ya Ziwa Victoria kuchukua tahadhari mvua na upepo mkali.

Kwa mujibu wa Wembe, tahadhari hiyo inatokana na utabiri iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu uwezekano wa ukanda wa Ziwa Victoria kupata mvua nyingi utakaoambatana na upepo mkali ndani ya siku tano zijazo.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here