Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Gissima Nyamo Hanga kwa kumtaka ahahakikishe anasimamia ukarabati wa mitambo ya umeme inayosababisha changamoto ya uwepo wa mgao wa umeme nchini.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa baada ya kipindi hicho hatakuwa tayari kusikia suala la mgao kwa kuwa suala la umeme linagusa maisha ya kila siku ya Watanzania.
Hayo ameyasema leo Septemba 26, 2023, Ikulu jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya uapisho wa viongozi aliowateua hivi karibuni ambapo aliweka wazi kwamba baada ya miezi sita ya utekelezaji wa maagiyo hayo hataki kusikia tena shida ya umeme.
“Nenda kaanzie pale Maharage alipofikia, najua utaweza, nakupa miezi sita nakuangalia pale TANESCO, kazi yako ya kwanza ni kusimamia ukarabati wa hiyo mitambo.
“Tuna changamoto kama taifa si ya mtu, mtu mwingine anaweza kusema Maharage kwa sababu ya kukatika katika kwa umeme kaondoshwa, hapana si sababu yake,” amesema Rais Samia.
Mkuu huyo wa nchi ameeleza sababu inayosababisha uwepo kwa mgawo wa umeme ni kuwa kuwepo kwa mitambo ambayo kwa muda mrefu haijafanyiwa matengenezo.
“Ikiwa haitafanyikwa huduma mitambo hii kwa pamoja ni lazima mitambo mingine iwake mingine izime. Kwahiyo tuna upungufu wa umeme,” amesema Rais Samia.
SABABU ZA KUHAMISHA
Akitolea ufafanuzi uhamisho wa Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta, Maharage Chande ambaye alihamishwa kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kupelekea Shirika la Mawasiliano (TTCL) na jana kuteuliwa kuwa Postamasta Mkuu, amesema hali hiyo ni kawaida katika utendaji.
Amesema sababu ya kumtoa kiongozi huyo kutoka Shirika la Mawasiliano (TTCL) kwenda kuwa Postamasta Mkuu, kuwa ni baada ya kubaini kuwa kiongozi huyo ana biashara ndani ya shirika hilo.
“Niliona sekta ya TTCL ingekufaa zaidi … baadaye nikagundua una biashara ndani ya TTCL na kwasababu kampuni ile inafanya vizuri nikasema hapana, usiende pahala ambapo unafanya biashara nikaona sasa nikupe Uposta Masta Mkuu,” amesema Rais Samia, Ikulu jijini Dar es Salaam