–AWASHA UMEME KIJIJI CHA MUBABA NA NYANTAKARA, ATAKA UMEME UFIKE KWENYE HUDUMA ZA KIJAMII
TERESIA MHAGAMA NA GODFREY LULINGA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko, leo ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kagera ambapo katika siku ya kwanza ya ziara yake amewasha umeme katika Kijiji cha Mubaba na Nyantakara vilivyopo wilayani Biharamulo.
Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa Serikali na wakandarasi wa umeme vijijini, Dk. Biteko ameagiza kuwa, sehemu zinazotoa huduma za kijamii kama vile shule, visima vya maji na vituo vya afya zipewe kipaumbele katika kupelekewa umeme ili wananchi waweze kupata huduma bora.
“Haileti maana umeme kufika katika eneo fulani kama watoto wanasoma gizani, haileti maana umeme kufika hapa halafu kina mama wanajifungulia gizani, wala haina maana umeme kufika hapa wakati kunavyanzo vya maji na tunashindwa kuwapelekea maji watu wetu, ndio maana Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) anataka mfikiwe na umeme ili usaidie kuboresha huduma na kuchagiza shughuli za uchumi,” amesema Dk.Biteko
Pamoja na hali hiyo, Naibu Waziri Mkuu Dk.Biteko ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme na wawakemee watu wanaoiba miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo, mafuta ya transfoma kwani wanarudisha nyuma jitihada za kuwafikishia umeme wa uhakika wananchi.
Kuhusu wakandarasi wanaosimamia miradi ya umeme amesema kuwa, wahakikishe wanafanya kazi kadri ya mikataba inavyoelekeza na kwamba kama kuna changamoto zozote wazieleze kwa viongozi, lakini REA wakiona kuna mkandarasi ambaye hafanyi kazi kama inavyotakiwa, mkandarasi huyo aondolewe na awekwe mwenye uwezo.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema kuwa atasilimamia ipasavyo agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kudhibiti changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme ndani ya kipindi cha miezi sita.
“Agizo hili la Mheshimiwa Rais tutalisimamia na kuhakikisha shida hii ndani ya kipindi cha miezi tunaipunguza kwa kiasi kikubwa ili watanzania wapate umeme wa uhakika,”amesema Biteko
Kuhusu nishati safi ya kupikia amesema kuwa, Serikali inakuja na mpango utakaowezesha wananchi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa wa asili ambao una athari kwa afya na kuleta nishati safi ambapo REA inakuja na mpango unaojumuisha kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi kwani lengo la Serikali ni kuhama kutoka nishati isiyo safi na Kwenda kwenye nishati safi.