*AVAA VIATU VYA KATE KAMBA, MAKILAGI, HASNA MWILIMA, KAMATI KUU CCM YAMPA JUKUMU ZITO, DC LULANDALA NAYE KUONGOZA UVCCM
Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) imemteua Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Jokate Mwegelo, kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT).
Jokate sasa anakwenda kuwa Mtendaji Mkuu wa nane wa umoja huo wa wanawake, ambapo tangu ilipoanzishwa kwake ambapo makatibu wakuu waliotangulia kuongoza jumuiya hiyo muhimu ya CCM ni Leah Lupembe, Kate Kamba, Halima Mamuya, Hasna Mwilima, Amina Makilagi, Mwal. Queen Mlozi, Dk. Philis Nyimbi na sasa Jokate Mwegelo.
Hatua hiyo ya kupewa Jokate kama mtendaji mkuu wa jumuiya hiyo inatarajiwa kwenda kuifanya jumuiya kuwa na mchanganyiko ambao huenda ukasaidia kuwa mvuto machoni mwa watanzania kwa kuonekana inamchanganyiko wa wanawake wa kila rika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba Mosi, 2023 na Katibu Wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Edward Mjema, ilieleza kuwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyokutana katika kikao chake maalum, Oktoba 1, 2023, jijini Dar es Salaam, imefanya uteuzi wa makatibu wakuu wa Jumuiya za Umoja wa Wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Katika kikao hicho, Kamati Kuu kimemteua, Jokate Mwegelo, kuwa Katibu Mkuu wa UWT, kabla ya uteuzi huo, Mwegelo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.
Pia, Kamati Kuu imemteua, Fakii Raphael Lulandala kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM, kabla ya uteuzi huo Ndugu Lulandala alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Momba, mkoani Songwe.
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imemteua, Hamad Khamis Hamad, kuwa mgombea wa CCM wa nafasi ya Uwakilishi katika Jimbo la Matembwe.
“Aidha, Kamati Kuu imewashukuru na kuwapongeza wanachama wote wa CCM na wananchi kwa ujumla katika Jimbo la Mbarali kwa kumchagua mgombea wa CCM Ndugu Bahati Kenneth Ndingo, kuwa Mbunge wao katika uchaguzi mdogo uliofanyika Septemba 20, 2023,” amesema Mjema katika taarifa yake
Mjema amesema kuwa pia, Kamati Kuu imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na ziara aliyoifanya katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambayo ilikuwa ya mafanikio makubwa sana.
“Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine, Rais alikagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025, kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wananchi.
“Pia, Kamati Kuu kimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa namna anavyoiongoza serikali katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” Amesema Mjema