Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa shule mpya ya Sekondari Malolo iliyopo katika Wilaya ya Mpwapwa inayojengwa kupitia fedha za mradi wa SEQUIP kiasi cha zaidi ya Sh millioni 544 ambayo haijakamilika mpaka sasa.
Akikagua ujenzi wa shule hiyo Oktoba 11, 2023 amesema kuwa hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi licha ya fedha za uendeshaji kutolewa mapema Juni 15, 2023 na unatakiwa kukamilika Oktoba 30, 2023 lakini bado unasuasua na kuonesha unaweza usikamilike kwa wakati.
“Lazima muamue kutafuta mbinu mbadala ili tuweze kukimbizana na wengine, hakikisheni mnaweka mafundi kwa shifti usiku na mchana tena kwa kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja, natarajia nkirudi hapa nikute imekamilika sitarajii kukuta sababu ambazo hazina msingi maana kila siku mnakuwa na sababu,” amesema Senyamule
Mradi huo unajumuisha Jengo la vyumba viwili vya madarasa, Jengo lenye vyumba viwili vya madarasa pamoja na Ofisi moja, Jengo la Utawala, maabara za Kemia, Biolojia na Fizikia, Maktaba, chumba cha Tehama, matundu manne ya vyoo vya wavulana yakiwemo na huduma kwa watu wenye mahitaji maalum, matundu manne ya vyoo vya wasichana, kichomea taka na tanki la maji la ardhini.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Kata hiyo kutoa kushirikiano kwa Serikali pale mradi unapokuja sambamba na kupeleka watoto wao Shule ili kutekeleza dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Wakati huo huo, Senyamule amewataka wakazi wa Kata hiyo kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kuepuka kujihusisha na uharibifu wa mazingira kwa kuhusika na ukataji miti ovyo, uchomaji wa mkaa kwa matumizi ya shughuli za kibinadamu jambo ambalo linaweza kusababisha vyanzo vya maji kutoweka.
Pia Senyamule amezungumza na wananchi na kupokea kero za uharibifu wa mazingira na kuahidi kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais.
Naye,Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Sophia Kizigo amewaahidi wananchi wa kata hiyo kuwa atawapelekea wataalamu wa mazingira kwa lengo la utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira.
Kutokana na hali hiyo amewataka wananchi kuwapa ushirikiano wataalamu hao watakapofika katikakata yao na kuahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizoibuliwa.