Home KITAIFA TANZANIA YATOA UFAFANUZI UN KUTETEA HATUA ZA KUNUSURU UHIFADHI WA LOLIONDO, NGORONGORO

TANZANIA YATOA UFAFANUZI UN KUTETEA HATUA ZA KUNUSURU UHIFADHI WA LOLIONDO, NGORONGORO

Google search engine

Na MWANDISHI MAALUM

-NEW YORK, MAREKANI

TANZANIA imeshiriki mkutano mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa ulioanza 25 Septemba, 2023 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York, nchini Marekani ambapo imetumia mkutano huo kuelezea hatua za Serikali kunusuru uhifadhi na maendeleo ya wananchi katika Wilaya ya Ngorongoro.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Balozi Hussein Kattanga, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Katibu Mtendaji wa Tume ya UNESCO nchini Tanzania Prof. Hamisi Malebo na Zuleikha Tambwe ambaye ni Ofisa Mwandamizi katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ulilenga kujibu hoja ya Mwandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Watu wa Asili, Francisco Calì Tzay aliyeandika kuhusu walalamikaji waliofungua kesi ya ardhi namba 26 ya mwaka 2013 katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Arusha wakidai kurejeshewa ardhi ijulikanayo kama Shamba la Sukenya au Hifadhi ya Mazingira ya Enavisha yenye ukubwa wa ekari 12,167 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo Katibu Mtendaji wa tume ya UNESCO nchini Tanzania Prof. Hamis Malebo amesema wajumbe wa mkutano huo kuwa haikuwa sahihi Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadiliwa chini ya kipengele cha ajenda ya Watu wa Asili na kusisitiza msimamo wa Serikali Tanzania kuwa haina watu wa asili, ardhi ya asili wala ardhi ya mababu.

Amefafanua kuwa jumuiya ya kimataifa na wanaharakati wa haki za binadamu wanapaswa kuuelewa mfumo wa umiliki wa ardhi nchini Tanzania kabla ya kutoa madai yoyote kwa kuwa mfumo wa umiliki wa ardhi Tanzania hautambui ardhi ya asili, ardhi ya mababu wala ya jadi.

“Ardhi yote ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini na mtu anapewa haki ya kukaa kwa muda maalum katika ardhi…. kwa hiyo, ni makosa kudai kwamba Waamasai au kabila lolote Tanzania linamiliki ardhi au lina ardhi ya kikabila.

“Ukweli ulio wazi ni kwamba binadamu wanaoishi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wanaathiriwa na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, magonjwa ya kutoka kwa wanyamapori, mabadiliko ya mazingira na hali ya hewa katika eneo hilo,” alisisitiza Prof. Malebo.

Amebainisha kuwa, sayansi ya uhifadhi wa bioanuwai inaonyesha shughuli za binadamu wanaoishi ndani ya misitu ni vichochezi vinavyoongeza kasi ya uharibifu na upotevu wa bayoanuwai jambo ambalo linadhoofisha uhifadhi wa urithi na jitihada za kupunguza ongezeko la joto duniani.

Akiongelea changamoto za kiuhifadhi katika Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, Prof. Malebo alibainisha kuwa wafugaji wa kabila la Waamasai wa Tanzania hapo awali walikuwa ni watu wa kitamaduni, wakiishi katika maboma ya asili  na wakihamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine wakitafuta maji na malisho kwa mifugo yao.

Katika siku za hivi karibuni, wameonekana kubadili mtindo wa maisha yao ya kimapokeo na sasa wana mseto wa imani tofauti kama za kimila, Kikristo na Kiislamu, wanajenga makazi kudumu na ya kisasa nyikani, wanafanya biashara mbali mbali na wanaendesha magari ambapo baadhi ya shughuli hizo zinakinzana na shughuli za uhifadhi.

Mwaka 1959 kulikuwa na wafugaji takribani 8,000 waliokaa katika eneo la makazi la kilomenta za mraba 6.4. lakini kwa sasa eneo la makazi ndani ya Ngorongoro si chini ya kilometa za mraba 3,700 ukilinganisha na eneo lote la hifadhi ambalo ni kilometa za mraba 8,292 sawa na asilimia 44.6.

Amebainisha zaidi kuwa, ongezeko kubwa linaloendelea la idadi ya watu na mifugo katika eneo hilo ni hatari kwa mfumo wa ikolojia na hatimaye bioanuwai iliyobaki inaweza kutokomezwa na eneo lote kubadilishwa kabisa kuwa makazi ya binadamu katika siku za usoni.

Hali hii haiendani na ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 na Malengo yake ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kwamba ulimwengu unaweza kupoteza Hifadhi ya Ngorongoro na dunia isione tena uhamiaji mkubwa wa Nyumbu.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here