NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imewazawadia Wanafunzi Bora wa Mwaka wa Masomo ya Biashara wa 2022/23, waliohitimu katika Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambako wanachuo wanne wamejizolea kiasi cha Shilingi Milioni 20, sawa na Sh. Mil. 5 kila mmoja.
Hafla ya kuwazawadia wanafunzi hao imefanyika UDSM, ambako Mkuu wa Kitengo cha Rasirimali Watu – Huduma Shirikishi wa NMB, Joseph Ngalawa, aliwakabidhi kila mmoja hundi ya mfano ya kiasi hicho, mbele ya Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye.
Tuzo na zawadi hizo ni sehemu ya makubaliano yaliyosainiwa mwaka jana baina ya NMB na UDSM, ambako taasisi hiyo ya fedha itakuwa ikiwazawadia Wanafunzi Bora wa Degree ya Kwanza kwa Masomo ya Biashara wa chuo hicho kwa miaka miwili mfululizo.
Kulingana na makubaliano hayo ya mwisho wa mwaka jana, NMB ilipaswa kuwazawadia wanafunzi watatu bora, lakini kutokana na wanachuo wawili kufungana katika ufaulu wao, ikalazimika kuwatunukia wanafunzi wanne.
Wanafunzi waliotwaa zawadi ya Sh. Milioni 5 kila mmoja na degree zao kwenye mabano ni; Zubeda Hemed Bakar (Bachelor of Commerce in Banking and Financial Services) na Rajab Fadhili Mchovu (Bachelor of Commerce in Finance).
Wengine ni Esther Charles Maboja na Tatu Rajabu Kikanda, ambao walifungana kwa ubora wa ufaulu katika Bachelor of Commerce in Accounting, hivyo NMB kuamua kuwatunukia wote na kufanya zawadi kufikia Sh. Mil. 20, walizopewa wakishuhudiwa na wazazi na walezi wao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Ngalawa alisema walisaini makubaliano hayo kwa lengo la kuwapongeza wanachuo wanaofaulu vema katika masomo yao, sambamba na kuchochea wanafunzi wengine waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao chuoni hapo.
“Tuko hapa kuwapongeza na kuzawadia wanafunzi waliofaulu vizuri zaidi katika mitihani yao ya kumaliza Degree ya Kwanza katika Chuo Kikuu cha UDSM, tukiamini kuwa kufanya hivi kutawachochea wengine nao kusoma kwa bidi na kupata ufaulu wao katika mwaka ujao.
“Huu ni muendelezo wa ushiriki wetu katika ngazi mbalimbali za elimu nchini Tanzania, ambako kwa Vyuo Vikuu tunazo program nyingi kwa ajili ya wanafunzi, zikiwemo ‘Internship Program na Field Students Program.’
“Programu hizo zinawapa uzoefu wanafunzi waliomaliza vyuo kuhimili ushindani wa soko la ajira, lakini pia tunayo ‘Management Trainee Program’ kwa ya wanafunzi wa Kitanzania wa vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, kupata mafunzo ya kuwa viongozi wa baadaye,” alisema Ngalawa.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Anangisye, aliishukuru NMB kwa kukabidhi zawadi hizo kwa wanafunzi wake kama walivyokubaliana na kwamba Sekta ya Elimu ya Juu inahitaji wadau wengi zaidi wa kuchagiza ufaulu na ustawi wa elimu kama NMB.
“Wako hapa kuwazawadia vijana wetu ikiwa ni sehemu ya makubaliano yetu ya mwisho wa mwaka jana, kufanya hivi kunaongeza chachu na ari ya kujisomea miongoni mwa wanafunzi, hivyo kuongeza ubora wa wahitimu wetu katika soko la ajira,” alisema Prof. Anangisye.
Naye Latifa Mbelwa ambaye ni Amidi wa Shule Kuu ya Biashara UDSM, alisema ili kukidhi ya kutoa huduma tatu UDSM, chuo kinahitaji washirika mfano wa NMB ili sio tu kuzawadia wanachuo bora, bali pia kukisaidia chuo chake kujua program shindani kwenye ajira ndani na nje ya nchi.
“UDSM tunatoa huduma tatu, za Utafiti ili kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, kutoa huduma kwa jamii na kujenga uwezo kielimu kwa maana kufundisha, ili kuzalisha wafanyakazi wanaoenda kuhudumu katika sekta za umma na binafsi.
“Kwa hiyo hili sio jukumu tu la chuo, bali na wadau wote ndio maana tunawapongeza NMB kwa makubaliano tuliyoyasaini mwaka jana, ambayo utekelezaji wake ndio huu,” alisisitiza Mbelwa, huku wanufaika wa zawadi za NMB nao wakiishukuru benki kwa pesa walizopewa.
Mwisho