Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
KATIKA Makala haya sehemu ya kwanza tuliangazia changamoto kadhaa katika Bandari yetu jambo ambalo kama Taifa lazima tuendelee kusimama pamoja ili kuona namna bora ya kupata mwekezaji ambaye atasaidia kuleta ufanisi bora na kuiweka bandari kwenye ushindani madhubuti.
Tanzania na mataifa jirani ya Afrika Mashariki yanatajwa kuwa yanaweza kuboresha pato la ndani la mwaka GDP kama yatachukua hatua za kuboresha ubora wa bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ripoti mpya iliyopewa kichwa cha ‘Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania’ iliyoandikwa na Jacques Morisset, mchumi mkuu wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Uganda na Burundi, Tanzania na majirani zake wanaweza kuongeza pato lao la ndani kwa kiwango kikubwa.
Ripoti hiyo inasema Tanzania inaweza kuongeza pato lake la ndani kwa kiasi cha dola bilioni 1.8 na nchi jirani zinaweza kupandisha pato la ndani kwa dola milioni 830 kwa mwaka, kiwango ambacho kinaelezewa ni hasara iliyotokea mwaka 2012.
Ripoti hiyo inasema kuwa Bandari ya Dar es Salaam iko katika njia kuu ya biashara ya Tanzania kwa asilimia 90, na inashughulikia bidhaa zinazogharimu dola bilioni 15 kwa mwaka, sawa na asilimia 60 ya pato la ndani la Tanzania kwa mwaka 2012.
Mwaka 2012 pekee, ripoti inasema hasara ya jumla inayoelezewa ambayo imetokea katika bandari hiyo imefikia dola bilioni 1.8 kwa uchumi wa Tanzania na dola milioni 830 kwa nchi jirani. Hasara ambayo ni sawa na asilimia saba ya pato la ndani la mwaka la Tanzania, na kwa kiasi kikubwa imeathiri wanunuzi wa ndani, biashara na mashirika ya serikali.
Moja ya sababu ambazo inaelezewa zimechangia katika hasara hii ni utendaji mbaya wa bandari ya Dar es Salaam ambao umezigharimu nchi nyingine jirani nazo kupata hasara, na hivyo kulazimika kulipa fedha zaidi kwa bidhaa zinazoagiwa kutoka nje, ikiwemo bidhaa za msingi kama vile mafuta ghafi, simenti, mbolea na madawa.
Matarajio ya ukuaji Shehena kwa kuzingatia uwepo wa mwekezaji
Kwa mujibu wa Mkataba (IGA), uwekezaji wa DPW utahusisha maboresho ya eneo la bandari, eneo la kuhifadhia mizigo, mifumo ya uendeshaji wa bandari na uwepo wa mitambo na vifaa vya kutosha.
Maboresho haya yanatarajiwa kuongeza shehena na mapato ya Kodi inayokusanywa na TRA kutokana na mzigo unaopitishwa bandari ya Dar es Salaam. Maoteo ya ongezeko hili yanatarajiwa kutoka tani milioni 18.41 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 42.6 ifikapo mwaka 2032/33.
Umuhimu wa kushirikisha Sekta Binafsi
Ili uchumi wa Taifa lolote duniani uweze kukua ni lazima kushirikisha wadau wa sekta binafasi kama njia pekee ya kusaidiana na Serikali katika kuleta ufanisi tarajali.
Na kutokana na hili kwa upande wa Bandari iwapo itashirikisha sekta binafasi yafuatayo yanatarajiwa katika kuleta matokeo Chanya nayo ni;
i.Kwa miaka saba mfululizo wastani wa ongezeko la kodi inayokusanywa na TRA kutokana na shughuli za kibandari imebaki kuwa asilimia 36.52; na
ii.Malengo ya Shehena kwa kipindi kama hicho hayakufikiwa kama ilivyopangwa ambapo ukuaji wake umekuwa chini ya asilimia 10 (wastani wa asilimia 4.36 kwa mwaka).
Hali hiyo ikiachwa kuendelea hivyo bila kufanya juhudi za makusudi kufanya mabadiliko, itasababisha nchi yetu kupata athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
i.Wateja kukimbia bandari za nchini kutokana na ufanisi mdogo na meli kuchukua muda mrefu kushusha na kupakia mizigo.
ii.Bidhaa zinazopita katika bandari zetu kuwa za ghali na hivyo, kusababisha kupeleka gharama kubwa kwa mlaji wa mwisho.
iii.Mchango wa mapato ya kibandari kutoongezeka na hivyo kufanya nchi kuendelea kutumia mikopo ambayo ni ghali katika kuhudumia wananchi wake.
iv.Uwezo wa bandari ya Dar es Salaam utafikia ukomo wa kutoa huduma na kuwa na tija ifikapo mwaka 2025/26; na
v.Upatikanaji wa fedha za kigeni na ajira. Kutokana na athari hizo, Wizara inaona upo ulazima wa kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha utendaji wa bandari zetu na kuingiza zaidi mapato nchini.
Manufaa yatakayopatikana kwa kuridhia IGA
Yapo manufaa kadhaa endapo kama Taifa tutaridhia mkataba wa IGA ikiwamo;
Kiuchumi
i. Kuwezesha ushirikishaji wa Sekta Binafsi wenye tija na utakaosaidia katika kupanua wigo wa shughuli za bandari na kuchangia ukuaji wa mapato ya Serikali na kuongeza fursa za ajira kwa watanzania
ii.Kuchochea sekta zingine za uzalishaji na viwanda kwa kuhakikisha bidhaa ghafi na zilizozalishwa zinafika kwa wazalishaji na walaji kwa wakati
iii.Kupunguza gharama za kufanya biashara pamoja na za usafirishaji kwenye mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka kwa wazalishaji kwenda kwa mlaji wa mwisho;
iv.Kupunguza gharama za bidhaa zinazoingizwa nchini kutokana na kuwa na gharama ndogo za bandari
v. Kuongeza fursa za Serikali kuwekeza katika maeneo mengine kutokana na rasilimali zitakazoonekana zimetokana na kutowekeza bandarini.
Kisiasa
i.Kuchangia katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi hususan katika kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika sekta mbalimbali za kiuchumi na hivyo kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja; na
ii.Kuimarisha uhusiano wa diplomasia ya uchumi na ushirikiano baina ya Serikali za Tanzania na Dubai.
Kijamii
Kuchochea upatikanaji wa huduma za kijamii kutokana na sera ya kurudisha faida kwa jamii (Community Social Responsibility- CSR)