Home KITAIFA NMB YAWANOA WAHARIRI UMUHIMU BIMA ZA AFYA, MAZISHI

NMB YAWANOA WAHARIRI UMUHIMU BIMA ZA AFYA, MAZISHI

Google search engine
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack wakimsikiliza Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng’ingo alipotembelea banda la benki hiyo katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi ambako kunafanyika Mkutano mkuu wa Saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Na MWANDISHI WETU

-BEST MEDIA, LINDI

BENKI ya NMB imewanoa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu matumizi ya huduma mpya za bima ya afya pamoja na bima ya mazishi ambazo zimetajwa kuwa mkombozi kwa Watanzania wenye kipato cha chini.

Hayo yamesemwa leo Novemba 13, 2023 katika Mkutano Mkuu wa Saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), unaofanyika mkoani Lindi.

Akiwasilisha mada kuhusu benki hiyo ambayo ni moja ya wadhamini wa mkutano huo, Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng’ingo, amesema kuwa huduma hizo zinalenga kuboresha afya za Watanzania.

Akifafanua kuhusu huduma ya Bima ya Afya ambayo inatolewa na benki hiyo kupitia Kampuni ya Strategis, Ng’ingo amesema wateja wa benki hiyo wanaweza kujiunga na huduma za bima ya afya kwa gharama ya Sh 200,000 pekee kwa mwaka.

“Hii sio bima ya mkoani tu. Unatibiwa hospitali zote za ngazi ya rufaa ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili,” amesema.

Ameongza kuwa kwa gharama hiyo ya Sh 200,000 inawezesha familia ya baba, mama na watoto wa nne kupata huduma hizo za afya.

Amesema iwapo kutakuwa na ongezeko la watoto, kila mmoja atatakiwa kulipiwa nyongeza ya Sh 80,000.

Ameongeza kuwa katika magonjwa sugu ya muda mrefu, bima hiyo itawezesha mgonjwa kutibiwa kwa muda wa mwaka mmoja.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma za bima ya mazishi, Afisa Uhusiano wa Benki ya NMB Mkoa wa Lindi, Christina Silayo amesema wanufaika wa huduma hiyo wanaweza kupewa mkono wa pole kuanzia Sh milioni moja hadi milioni tano.

Amesema huduma hiyo inapatikana kutokana na wanufaika kujiunga kwenye kikundi na kujipangia kiwango cha mchango kuanzia Sh 2000 hadi Sh 8,500.

Amesema mnufaika wa huduma hiyo ambaye pia anaweza kuwa msimamizi wa mirathi,  atapata mkono wa pole kwa kuwa na uthibitisho wa cheti cha kifo cha mteja aliyejiunga na huduma hiyo enzi za uhai wake.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here