Na MWANDISHI WETU
-LINDI
MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma PSSSF, umetoa elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 7 wa Jukwaa la Wahariri Tanzanai (TEF) mjini Lindi.
Akizunguza leo Novemba 14, 2023, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe, amesema hadi kufikia Septemba 9, 2023 uwekezaji wa Mfuko umefikia zaidi ya shilingi Trilioni 8.16.
Amesema mafanikio hayo ya uwekezaji ni ya kujivunia kwani ni makubwa ndani ya kipindi kifupi na yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuongeza ajira, kufungua nchi na kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Kwa upande wake Meneja Mafao wa PSSSF, Ramadhani Mkeyenge, amesema ukiacha jukumu hilo la Mfuko katika eneo la uwekezaji, Mfuko pia umetekeleza kwa mafanikio makubwa jukumu la Ulipaji Mafao.
Alisema Mfuko unatoa jumla ya Mafao saba ambayo ni pamoja na Fao la Uzeeni (Pensheni), Fao la Ulemavu, Fao la Kifo, Fao la Urithi, Fao la Uzazi, Fao la Kukosa Ajira na Fao la Ugonjwa.
Mfuko unalipa pensheni kwa Wastaafu 167, 937 na Wategemezi, wastani wa shilingi bilioni 67 kila mwezi.” Alifafanua Bw. Mkeyenge
“Mfuko tangu uanze kutekeleza majukumu yake mwaka 2018 hadi Juni 2023, umelipa kiasi cha shilingi trilioni 8.8 kwa wanachama wapatao 262,095.” Alisema na kuongeza…Kila mwezi pensheni inayolipwa kwa wastaafu na wategemezi ni wastani wa shilingi bilioni 67,” amesema