Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
BENKI ya NMB imesema imeanza kuzingatia kwa karibu masuala ya uhifadhi wa mazingira katika uendeshaji wake na kufadhili miradi mbalimabli kutokana na umuhimu wake katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wiki hii, Afisa Mwandamizi wa Benki ya NMB , Hellen Dalali, amesema kutokana na hilo NMB sasa inaipa kipaumbele miradi rafiki kimazingira na wakopaji wanaolitambua hilo.
Dalali aliuambia mkutano kuhusu suluhisho asilia (NBS) dhidi ya janga la mabadiliko ya tabianchi kuwa ufadhili unaofanywa na benki hiyo umejikita zaidi kupunguza athari za hewa ukaa na kuongezeka kwa joto duniani.
Amesema NMB imeweka msimamo huo kutokana na umuhimu wa miradi ya kijani na ile yenye tija kijamii kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo endelevu.
Aidha, Meneja Miradi Mwandamizi huyo alibainisha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi si tu ni hali halisi iliyopo bali pia ni hatari kubwa ambayo madhara yake tayari yanaziyumbisha biashara na chumi nyingi duniani.
Akizungumzia athari za janga hilo wakati wa jopo la utangulizi la mkutano huo, amesema sekta ya fedha nayo tayari imeahirika hivyo kuongeza umuhimu wake kushiriki na kuwekeza vilivyo katika hatua za kupambana na changamoto hizo.
“Hakuna hata mmoja wetu ambaye hajaathirika kwa hiyo wote tunawajibika kushiriki kikamilifu kupambana na athari hizi,” Dalali amewaambia washiriki wa Mkutano wa NBS Tanzania 2023, ambao ulilenga hasa maendeleo ya biashara ya hewa ya ukaa nchini.
Amesema hatari za mabadiliko ya tabianchi zimeilazimu NMB na benki nyingine kubuni mbinu mpya za kibenki na uendeshaji ili kupunguza kaboni hewani na kukidhi matarajio ya kuhifadhi mazingira.
“Mabadiliko ya tabianchi yameathiri biashara nyingi duniani na kupekea chumi nyingi na sekta ya fedha kuathirika vile vile kutokana na biashara hizi kufadhiliwa na benki,” alibainisha.
Kwa mujibu wa Dalali, benki hazijikiti tu kupunguza shughuli zake kuathiri mazingira bali pia zinaongeza umakini katika tathmini za athari za kitabianchi na kijamii kwenye michakato ya mikopo.
Hilo linafanyika kuunga mkono juhudi za kitaasisi kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha miradi na biashara zinazofadhiliwa zinakuwa na madhara madogo au haziathiri kabisa mazingira, alifafanua.
Ameongeza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa benki zipo za aina mbili, moja ikiwa ni zile zinatokana na uharibifu wa mali na rasilimali kutokana na majanga kama mafuriko au mvua kubwa.
Kundi la pili ni lile la athari za kimpito ambazo hasa zinatokana na madiliko ya kikanuni, kisera, kiteknolojia na kimasoko yanayolenga kuchagiza shughuli za kiuchumi zinazozalisha hewa kidogo ya ukaa na kupambana na changamoto nyingine za mabadiliko ya tabianchi.
Dalali ameuambia mkutano huo wa siku moja kuwa pamoja na athari zake nyingi, mabadiliko ya tabianchi pia yana fursa lukuki za kibiashara, ambazo mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo, Waziri Angela Kairuki, alisema ni pamoja na biashara ya hewa ukaa ambayo inazidi kuimarika nchini.
Akitolea mifano ya hatifungani ya NMB Jamii Bondi na kampeni ya kupanda miti iliyozinduliwa na benki hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, mtaalamu huyo wa masuala ya uendelevu alisema benki zinaweza kuongoza kuzifungua fursa hizo kupitia ufadhili endelevu na ule wa kijani.
“Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatoa fursa na mazingira muafaka ya biashara kwa sekta binafsi na benki kushiriki. Hii ni kupitia uhamasishaji stahiki wa fedha na mitaji ili kuweza kufadhili miradi ya kukabiliana na changamoto hizo,” alibainisha na kusisitiza umuhimu wa uwezeshwaji kimaarifa ili kuwa na kada yenye ufahamu mzuri wa ufadhili wa aina hiyo.
Suala jingine, ambalo alisema ni nyeti katika kuishirikisha sekta binafsi katika masuala ya tabianchi, mijadala ya biashara ya hewa ukaa na mipango ya masuluhisho asilia, ni lile la ushirikiano kama ambavyo NMB imefanya na Wakala wa Misitu Tanzania kwenye mradi wa kupanda miti milioni moja nchi nzima mwaka huu.