Home KITAIFA MWENYEKITI WA BODI YA NISHATI VIJIJINI AAGIZA MIRADI YOTE IKAMILIKE KABLA YA...

MWENYEKITI WA BODI YA NISHATI VIJIJINI AAGIZA MIRADI YOTE IKAMILIKE KABLA YA DESEMBA 2023

Google search engine

*ATAKA WAKANDARASI KUHAKIKISHA UBORA NA WELEDI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Mtwara (hawapo pichani). Kikao hicho kilifanyika mkoani humo na kililenga kujadili mikakati ya pamoja kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kwa ubora.
Mmoja wa Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Thomas Uiso, Mkurugenzi wa Kampuni ya Ukandarasi ya Namis Corporate Ltd, akieleza mikakati yao mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu (Meza Kuu) itakayowezesha kukamilisha miradi kwa wakati katika kikao kilichofanyika mkoani humo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu (Meza Kuu) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Mtwara. Kikao hicho kilifanyika mkoani humo na kililenga kujadili mikakati ya pamoja kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kwa ubora.

Na Veronica Simba, Mtwara
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Wilaya za Nachingwea, Nanyumbu, Masasi na Tandahimba kukamilisha miradi
yao ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Pia amewaelekeza kuhakikisha ubora, weledi  na kukamilika kwa wakati miradi yote wanayoisimamia ili wananchi wapate huduma kwa muda uliopangwa.

“Nishati ni kila kitu, usalama, uchumi, siasa, afya na maeneo mengi, hivyo, jukumu la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni kuhakikisha kuwa wanawapatia wananchi umeme ili waweze kutimiza malengo yao,” amesema Balozi Kingu.

Amesema hayo katika kikao chake na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nishati vijijini katika Mkoa wa Mtwara ambapo amewataka watendaji wa REA na TANESCO kuwafuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa lengo la
kuvifikia vijini vyote ifikapo Juni 30, 2024 linafikiwa.

Wakandarasi hao , NAMIS Corporate Ltd na Central Electrical International Co, wametakiwa kuongeza nguvukazi na upatikanaji wa vifaa kwa wakati ili ifikapo Novemba 30, 2023 vijiji vyote walivyopangiwa kimkataba viwe
vinawaka umeme.

Amewaagiza kutumia vifaa vinavyozalishwa  na kupatikana katika viwanda vya ndani ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuagiza nje vile tu ambavyo havipatikani nchini.

Ametaka kikao cha tathmini kifanyike Desemba Mosi mwaka huu  na wakandarasi hao na kuona kama wako katika muda uliopangwa na endapo kuna changamoto waone namna bora ya kuzitatua kwa pamoja.

Pia amewataka Wakandarasi kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa kazi zao kila wiki ili kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amempongeza Balozi Kingu kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais Samia katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi na kuongeza kuwa anaamini kwa sifa yake ya uchapakazi, REA itaendelea kupata matokeo chanya zaidi.

Kanali Ahmed amesema anatamani kuona wananchi wote wa vijijini wanafikiwa na umeme kama ilivyodhamiriwa na Serikali ili waweze kuboresha maisha yao na kwamba hana shaka kuhusu kutimia kwa jambo hilo ikiwa wote wanaohusika watashirikiana.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Mtwara, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu alisema hadi sasa, vijiji 384 kati ya 785 vimekwishafikishiwa huduma ya umeme na kwamba kazi inaendelea ili kukamilisha vijiji vyote.

Mhandisi Olotu ambaye ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, amesema Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (R3-R2) ambao ni mojawapo ya miradi inayoendelea kutekelezwa mkoani humo unalenga kufikisha umeme katika vijiji vyote 401 na kwamba Wakandarasi wanaendelea na kazi hiyo.

Aidha, ametaja miradi mingine inayoendelea kutekelezwa mkoani humo kuwa ni pamoja nan a Mradi wa Vijiji Miji, Mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo ya madini, maeneo ya kilimo, vituo vya afya na pampu za maji pamoja na Mradi wa Ujazilizi.

“Hadi kufikia Novemba 15 mwaka huu, REA imewasha umeme katika vijiji 193 kati ya 401 ambavyo vilikuwa havina umeme kwa Mkoa wa Mtwara wakati Mradi wa R3-R2 unaanza kutekelezwa Julai, 2021.”

Mhandisi Olotu ameongeza kuwa, vijiji 208 vilivyobakia vitafikishiwa umeme kabla ya Juni 2024.

Akizungumza kwa niaba ya Wakandarasi wenzake, Mhandisi Thomas Uiso, Mkurugenzi wa Kampuni ya Ukandarasi ya Namis Corporate Ltd, ameahidi kwamba watafanya kazi kwa bidi ili kukamilisha yale yote waliyoelekezwa.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka REA, Mussa Muze pamoja na Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Daniel Mwandupe pamoja na viongozi mbalimbali wa TANESCO Mtwara.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here