Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema Watanzania wana kiu ya kuona ukumbi wa Kimataifa wa Michezo ( Sports Arena) inajengwa nchini huku akieleza kwamba tayari Wizara imepokea hekari 12 eneo la Kawe jijini Dar es salaam kwa ajili ya ukumbi huo.
Akizungumza leo Februari 14, 2023, Waziri Mohamed Mchengerwa wakati akikabidhiwa hekari hizo 12 , amesema kuwa Sports Arena itakayojengwa Kawe utakuwa na uwezo wa kubeba watu 16000 na hivyo kutoa nafasi pia ya Watanzania kushuhudia matamasha mbalimbali yatakayokuwa yakifanyika katika ukumbi huo.
Aidha, Waziri Mchengerwa ameeleza kwamba dhamira ya Dk. Samia Suluhu ni kuhakikisha sekta ya burudani na michezo zinakuwa sekta zinazokwenda kuchangia pato la Taifa.
“Watanzania wamekuwa wakihoji kuwa tayari Bajeti imepitishwa lakini hawaoni utekelezaji wa ujenzi wa ukumbi huo, lakini tuwatoe hofu kuwa sasa tunaenda kuandika historia nchini Tanzania kujengwa kwa ukumbi huo wa Kimataifa,” amesema Waziri Mchengerwa.
Pia ameeleza Arena hiyo inatarajiwa kukamilika kati ya Agosti na Oktoba mwaka huu na utakuwa moja ya ukumbi mkubwa barani Afrika kama ilivyo Arena kubwa ya nchini Senegal inayochukua watu 15000.
“Tulipotoka hatukuwa na mipango mizuri hivyo tulivyoingia na Wasaidizi wetu tumehakikisha tunaenda kuongeza nguvu kubwa tutengeneze mipango yetu, tutengeneze michoro na hatua zote tumekwisha kuzikamilisha na tunatarajia mwezi Machi mwaka huu kumkabidhi Mkandarasi na ujenzi.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba Wizara itahakikisha inasimama kidete hadi kukamilisha maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kukamilisha ujenzi huo wa ukumbi wa Arena nchini Tanzania.