*Azungumzia milima, mabonde katika kuijenga chama, amtaja Maalim Seif, abakiza saa chache kung’atuka kwenye uongozi wa chama
*Agusia maisha ya Rais Mstaau Ali Hassan Mwinyi
Na MWANDISHI WETU, BEST MEDIA
-DAR ES SALAAM
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameweka wazi kwamba sasa anaondoka ndani ya uongozi wa chama hicho bila huku akiicha kama taasisi ambayo haitegemei kujengwa kwa majina ya watu.
Hayo ameyasema leo Machi 4, 2024 katika mahojiano maalumu yaliyorushwa kituo cha redio cha Clouds FM kupitia kipindi cha Power Breakfast, ambapo amesema kuwa ACT Wazalndo, kimeweka utaratibu wa kubadilishana uongozi ambapo kupitia utaratibu huo wanaamini kutaimarisha demokrasia na kuwa na taasisi imara nyakati zote.
“Sisi kama ACT Wazalendo tumeweka utaratibu wa kubadilishana uongozi na tunaamini kwamba mkiweka huo utaratibu chama kitaweza kuimarika kitaasisi, chama hakitatambulika kwa mtu, nyinyi mnafahamu kwamba sasa hivi ukienda mtaani mtaambiwa kwamba bila Zitto Kabwe hakuna ACT Wazalendo.
“Na tulikuwa tunaambiwa kwamba Maalim Seif Sharif Hamad (aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais SMZ) amefariki na ACT Wazalendo imekufa na haitakuwepo lakini tumeweza kuwepo na tumeendelea kukua kwa kasi zaidi,” amesema Zitto
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa anaondoak kwenye uongozi wa chama na chama hicho kinapaswa kuendelea kuwepo kwani yeye na wenzake muda wote walijitahidi kukitengeneza kama taasisi ambayo ni zaidi ya mtu mmoja.
“Sasa hivi Zitto Kabwe anatoka kwenye uongozi na chama kinapaswa kuendelea kuwepo, sisi tunajitahidi kutengeneza taasisi ambayo ni zaidi ya mtu mmoja, sasa inawezekana kwamba vyama vingine wao hawaoni kama ni jambo ambalo lina manufaa kwao, kwa hiyo ni vigumu sana mimi (Zitto Kabwe) ambaye ni kiongozi wa chama kingine kutoa maoni kuhusiana na taratibu za vyama vingine na ukitaka hayo maoni inabidi uwaite na uwaulize wao,” amesema
Zitto ambaye amewahi kuwa Mbunge katika majimb ya Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini kwa nyakati tofauti, amesema kuwa hata hatua ya chama hicho kufikia kuwa na midahalo kwa wagombe wake wa nafasi mbalimbali kama njia ya kuimarika kwa demokrasia ndani ya chama hico na inaonesha ni tofauti na Chama tawala CCM ambao alidai hukwepa midahalo.
“Leo tutakuwa na midahalo ya wagombea wa nafasi zote za juu na tunafanya hivi kwa sababu huku nje nyakati za chaguzi kubwa tunalalamikia kwamba CCM wanakimbia midahalo, hawataki midahalo na sisi tunataka tukutane nao kwenye midahalo, huku ndani lazima na nyie muonyeshe mnayaishi hayo?.
“Yaani muwe mfano, tumeamua kujenga taasisi yetu (ACT Wazalendo) kwa misingi ile ambayo tunaipigania nje, tuipiganie na ndani. Huwezi kusema watu wanakaa madarakani muda mrefu lakini wengine ila sio wewe, au kusema kwamba hamna demokrasia lakini ndani wewe huangalii demokrasia, nje ndio unaangalia demokrasia, tumesema hapana tunataka tujenge demokrasia kwa mujibu vile ambavyo tunataka na ndio haya ambayo mnayashuhudia ndani ya ACT Wazalendo katika kipindi hiki cha wiki nzima,” amesema Zitto
KUHUSU MZEE MWINYI
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo, amesema kuwa mapema hivi karibuni Taifa limempoteza alikuwa Rais wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi na kumtaja kama Baba wa Mageuzi nchini.
“Mzee Hayati Ali Hassan Mwinyi alikuwa Baba wa mageuzi kwa sababu kuna mageuzi makubwa mawili ambayo yamefanyika nchini kipindi cha uongozi wake, muhula wake wa kwanza ilikuwa ni marekebisho ya uchumi, mageuzi ya kiuchumi ambapo hali ya kiuchumi ilikuwa ni mbaya sana, wakati Mzee Mwinyi anakuwa Rais nilikuwa darasa la pili, shule ya msingi Kigoma.
“Ukisikia watu wakizungumzia ugumu wa maisha, pamoja na kwamba nilikuwa mdogo lakini niliona, kwa sababu nakumbuka nilikuwa nakwenda shuleni bila viatu, kulikuwa hakuna bidhaa kwenye maduka, siku ukibahatika kunywa uji ilibidi unywe uji wa chumvi, hakukuwa na sukari madukani, sasa hivi watu wanalalamika kuhusu biashara ya sukari enzi hizo sukari yenyewe haikuwepo,” amesema
Rais Mwinyi ambaye amefariki, Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar e Salaam, akiwa na umri wa miaka 99 ambapo amezikwa kijijini kwao Mangapwani visiwani Zanzibar Machi 2, 2024.
SAFARI YAKE NDANI YA MAGEUZI
Zitto ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo na amehudumu kama Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini katika Bunge lililomaliza muda wake la 11.
Zitto ni mchumi kitaaluma, akiwa ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Zitto pia alisomea Biashara ya Kimataifa kutoka Went-Trade Africa Programme (Bonn, Ujerumani) na ana Shahada ya Uzamili kwenye Sheria na Biashara aliyoipata kutoka Shule ya Sheria ya Bucerius (Humburg, Ujerumani).
Mwezi Julai, 2015, jarida maarufu ulimwenguni la masuala ya biashara la Financial Times lilimtaja Zitto kwenye orodha yake ya watu 25 wa Kiafrika wa kuwaangalia.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ni miongoni mwa waliokumbana na tuhuma za kufanya usaliti kwa kuandaa mapinduzi ya uongozi akiwa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Novemba 23, 2013 Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa aliyekuwa Kaibu Mkuu wake wa wakati huo, Dk. Wilbroad Slaa, alitangaza kuwavuliwa kwa nyadhifa zao, aliyekuwa Naibu Katiu Mkuu wa chama hico Tanzania Bara, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu ka wakati huo Profesa Kitila Mkumbo.
Kwenye maamuzi hayo Kamati Kuu imesema kuwa Zitto na Kitila wanatuhumiwa kwa kufanya harakati za kutaka kukihujumu chama hicho pamoja na kwenda kinyume na maamuzi ya chama na mwenendo wake.
Dk. Slaa, mesema hata kama mtu ataamua kuondoka ndani ya chama hicho,kamwe hakitatetereka.
Hata kutokana na hali hiyo Zitto, alianza harakati za kuanza kuanzisha chama kipya ambapo kwa wakati huo kilijulikana kwa jina la ACT Tanzania na kisha baadaa ya yeye kujiunga na wenzake alibadili jina na kuiita ACT Wazalendo na kuweza kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kumuweka Anna Mghwira kuwa mgombea wake huku Zitto akitupa karata yake katika Jimbo la Kigoma Mjini na kufanikiwa kushinda kupitia ACT Wazalendo