Home KITAIFA Somalia nchi ya nane kujiunga Jumuiya ya Afrika Mashariki

Somalia nchi ya nane kujiunga Jumuiya ya Afrika Mashariki

Google search engine
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Muohamud (kulia) alipotia saini mkataba wa nchini yake kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kushoto ni Mwenyekiti wa zamu wa Jumuiya hiyo ambaye pia ni Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir. Katikati ni Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Peter Mathuki. Halfa hiyo ilifanyika mwaka uliopita mjini Kampala kabla ya hati hizo kuwasilishwa Machi 04, 2024 mjini Arusha

*Sasa EAC kukua hadi Dola Bilioni 3 na kuongeza soko la ajira

Na MWANDISHI WETU

-ARUSHA

SASA rasmi kwa nchi ya Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, hatua ambayo inatajwa ni ya kupigiwa mfano kwa Bara la Afrika kwa kuwa na muungano wa nchi unaokuwa.

Somalia inakuwa ni nchi ya nane kujiunga EAC huku wananchi wengine ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hatua hiyo inakwenda kuandikwa kwa historia mpya, ambapo Machi 4, 2024 Somalia iliruhusiwa rasmi kujiunga na jumuiya hiyo ikiwa sambamba na kupandishwa kwa bendera ya Taifa hilo kama ishara ya kuongezeka kwa mwanachama mwingine ndani ya EAC.

Aidha imeelezwa kuwa itasaidia suala zima la msukumo wa changamoto za ajira kwa nchi wanachama wa EAC kwa kuweka usalama hususani katika masuala ya biashara.

Umuzi huo ulitokana na kikao cha wakuu wa nchi za EAC kilichoketi Julai 22, 2023 na kamua kukubali ombi la Jamhuri ya Somalia kuwa mwanachama wa EAC.

Akizungumza Jijini Arusha katika sherehe fupi za kupandisha bendera na kupokea hati ya uanachama, Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Peter Mathuki amesema soko la Jumuiya limeongezeka na kuwa na watu takribani milioni 350 kwa sasa.

Amesema kiwango cha ukuaji wa pato la EAC limeongezeka kutoka Dola Bilioni 2.5  hadi Dola Bilioni 3 na kuongeza soko la ajira kuondoa changamoto za ukosefu wa ajira kwa nchi wanachama na ongezeko la bidhaa .

Akizungumzia suala la usalama Dk.Mathuki amesema kuwa kuongezeka kwa soka hilo la watu milioni 350 kutaondoa changamoto za upungufu wa ajira na kupelekea wananchi kuchangamkia uzalishaji wa bidhaa kuuza katika soko hilo.

“Hii ni moja ya kuondoa changamoto za ajira na kurudisha hali ya usalama katika mataifa ya EAC ikiwa soko la Jumuiya kwa sasa lina watu takribani milioni 350 uzalishaji wa bidhaa utaondoa upungufu na kuzalisha ajira hivyo kuwepo kwa usalama katika nchi zetu,” amesema Dk. Mathuki

Kwa upande wake Waziri wa Habari wa Somalia, Daud Aweso amesema wanayofuraha kukamilisha safari ndefu ya miaka 12 ambayo ilikuwa na kazi kubwa pamoja na changamoto lakini hawakuchoka kufikia hatua hiyo ya kukamilisha utaratibu wa mwisho wa kujiunga na EAC.

Amesema jumuiya hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa Somalia na nchi zote wanachama kwa kuwa nchi ya nane kujiunga.

Amesema kuwa changamoto zilizopo ndani ya Somalia wataendelea kuzifanyia kazi ambao kwa mwaka uliopita kuna mambo kadhaa waliyoyafanya ili kuhakikisha wanatoa picha halisi kwa wanachama zaidi ya milioni 350 wa EAC.

MOGADISHU KUTUMIA  FURSA NA KUKUZA UTENGAMANO KIKANDA

Somalia ni Taifa la pembe ya Afrika inajivunia ukanda wa Pwani mrefu zaidi barani Afrika, wenye urefu wa zaidi ya kilometa 3000 na kwamba eneo hilo linaweza kutumika kama rasilimali ya kukuza uchumi wa bluu na kuongeza biashara ya kikanda ndani ya Jumuiya.

Akizungumza katika hafla  hiyo, Mkuu wa ujumbe wa Somalia, Waziri wa  Biashara na Viwanda wa Somalia, Jibril Abdirashid Haji Abdi, amesema taifa lao lina shauku ya kuchangia kuikuza Jumuiya hiyo hasa kwa mambo ya mtangamano kwa kutumia eneo lake la kimkakati na rasilimali za Taifa kwa manufaa ka kanda nzima.

“Tunatambua umuhimu wa kuongeza thamani kwa Jumuiya, kuimarisha ushirikiano na jirani zetu na kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii na programu za miradi ya pamoja,” amesema Haji Abdi.

Maombi ya Somalia kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki, yaliwasilishwa na rais wa nchi hiyo, Hassan Sheikh Mahmoud, wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha, Julai 22 mwaka  2023.

Kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi nyingine inaweza kujiunga na jumuiya hiyo, endapo itaungwa mkono na nchi wanachama.

Vilevile iwapo nchi inayoomba itakuwa imetimiza masharti ya uongozi bora, demokrasia, inaheshimu sheria na haki za binadamu na kwamba iwe inapakana na miongoni mwa nchi wanachama.

Somalia inakadiriwa kuwa na idadi ya watu wanaofikia milioni 17 na kujiunga kwake na jumuiya ya Afrika Mashariki kunaifanya jumuiya hiyo kuwa na jumla ya mataifa nane. Mataifa mengine wanachama ni Tanzania, Kenya na Uganda ambazo ndiyo waanzilishi wa jadi wa jumuiya hiyo.

Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilijiunga baadaye.

Hali hafifu ya usalama nchini Somalia ni miongoni masuala yanayoweza kuibua wasiwasi wakati taifa hilo linaanza safari rasmi ya uanachama ndani Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here