Na MWANDISHI WETU
-NGORONGORO
KAMISHNA wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Richard Kiiza amefanya ziara katika baadhi ya vijiji vilivyoko ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kukagua maendeleo ya timu ya uelimishaji na uandikishaji wa wananchi wa tarafa ya Ngorongoro wanaojiandikisha kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi hiyo.
Akiwa kwenye ziara katika Vijiji vya Kayapusi na Oloirobi vilivyopo kata ya Ngorongoro, Kamishna Kiiza amekutana na moja ya timu inayoendelea na zoezi la uandikishaji na kuelezwa kuwa wananchi wameendelea kuhamasika na kujiandikisha kwa hiari hasa baada ya kupata elimu ya faida na hasara za kuishi ndani ya hifadhi na kupata taarifa za fursa lukuki za ndugu zao waliokwisha hama ndani ya hifadhi.
Akizungumza na baadhi ya wananchi aliokutana nao Kiiza amewaeleza kuwa Serikali hailazimishi mtu kuhama isipokuwa inamuelimisha hasara za kuishi ndani ya hifadhi ambapo sheria inazuia kufanya baadhi ya vitu ukilinganisha na mazingira anakoenda ambapo serikali imeboresha mazingira kwa kujenga miundombinu ya maji, shule, barabara, umeme, mawasiliano, eneo la malisho, minada na soko la maziwa.
Ameongeza kuwa wananchi ambao wangependa kwenda kuona maeneo yaliyoandiliwa na Serikali kabla ya kuamua kuhamia wana uhuru wa kufanya hivyo ili kukagua maeneo yaliyoandaliwa katika vijiji vya Msomera, Kitwai na Saunyi na serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano.
“Serikali haiwezi kuwa na nia mbaya kwa watu wake, ndio maana inajenga miundombinu yote muhimu, inawapa wananchi wanaohama fedha za motisha zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, sambamba na kuwapa fidia ya maendelezo waliyofanya wakiwa ndani ya hifadhi na kuwahamishia thamani na mifugo yao yote kwenda maeneo waliyochagua kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni na haki za binadamu,” amefafanua Kiiza.