Home KITAIFA ANTAKAE, KIZERUI WAOMBA UDHIBITI MABADILIKO YA TABIANCHI

ANTAKAE, KIZERUI WAOMBA UDHIBITI MABADILIKO YA TABIANCHI

Google search engine

Na Selemani Msuya
SERIKALI imeshauriwa kuongeza kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yameanza kuleta athari kwenye sekta ya kilimo na afya kwa wakulima mazao ya viungo yanalimwa eneo linalozunguka Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani wilayani Muheza mkoani Tanga.
Ushauri huo umetolewa na wakulima wa vijiji vya Antakae na Kizerui wakati wakizungumza na waandishi wa habari wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ambao wametembelea vijiji hivyo vinalima mazao ya viungo kwa njia ya kilimo hai.

JET imeratibu ziara hiyo ya waandishi kupitia ufadhili wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili ambapo wakulima wa mazao ya viungo wameeleza namna mabadiliko ya tabianchi yameaza kuwaathiri sekta ya kilimo na afya, hali ambayo inaweza kupunguza uzalishaji na maradhi kwa mimea na binadamu.
Akizungumzia changamoto hiyo Katibu wa Kamati ya Matumizi Bora ya Ardhi kijiji cha Kizerui kilichopo Hifadhi ya Amani-Nilo, Wilfred Seng’andu kwa miaka ya hivi karibuni wameshuhudia mabadiliko makubwa ya tabianchi, hivyo wanaishauri serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana nayo.
Seng’andu amesema wamekuwa wakikabiliana na wadudu waharibifu kwenye mazao ya viungo jambo ambalo huko nyuma halikuwepo na baada ya kufuatilia kwa watalaam wa kilimo wameambiwa hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatokea duniani.
Katibu huyo amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeonekana hadi kwenye afya za binadamu kwani kwa sasa wameshudia mbu jambo ambalo awali halikuwepo, hivyo kusababisha magonjwa ya malaria.
Amesema asilimia kubwa ya wakazi wa kijiji cha Kizerui wamekuwa wakijihusisha na kilimo cha mazao ya viungo kama karafuu, pilipili manga, mdalasini na iliki ambayo yamekuwa yakistawi kutokana na uwepo wa hali ya hewa nzuri na ardhi yenye rutuba, ila kwa miaka ya hivi karibuni hali imebadilika.
“Tunaomba Serikali iongeze kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo imeanza kutuathiri sisi wakulima wa viungo ambao tunatumia njia ya kilimo hai, kwani kuna hatari ya kutumia viuatilifu vya madukani ambavyo havikubaliki katika soko la dunia,” amesema.
Ametaja athari zingine ambazo wamekutana nazo kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni uzalishaji kuwa mdogo akitolea mfano mti mmoja wa karafuu unapaswa kutoa zaidi ya kilo 15, ila hali inapelekea kupata chini ya hapo, hivyo mkulima kuathirika.
Katibu huyo amesema wataalamu wa kilimo waliwahi kufika katika kijiji hicho na kuchukua ‘sample’ kwa ajili ya kufanyia kazi, hivyo wanasubiri majibu ya utafiti walioufanya kukabiliana na changamoto hiyo.
“Yaani haya mabadiliko ya tabianchi yamesababisha magonjwa ya mnyauko, wananchi kuwashwa, mbu na mengine ambayo kwetu tulikuwa tunasikia tu,” amesema.
Seng’andu amesema ujio wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), umeanza kusaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Kizerui, Avodia Baruti amesema miradi ya uhifadhi inayotekelezwa kijijini hapo imekuwa ikiwasaidia kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuiomba Serikali kuongeza kasi zaidi.
Magreth Seguni amesema kilimo cha mazao ya viungo kinalipa, ila changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuwakatisha tamaa, iwapo hakutakuwa na jitihada za haraka za kukabiliana na hali hiyo.
Naye Upendo Mzava wa kijiji cha Antake amesema serikali inapaswa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wakulima wa mazao hayo, ili wasipate athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Naamini Serikali ikiweka mkazo katika kilimo hiki, hizi changamoto za mabadiliko ya tabianchi zitapata ufumbuzi wa haraka na sisi wakulima tutakuwa salama,” amesema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Antakae, Hamza Magembe amesema serikali ya kijiji imekuwa ikitoa taarifa za mabadiliko ya tabianchi kila wakati, hali ambayo imeongezea uelewa wakulima na wananchi kwa ujumla, huku akiwapongeza USAID Tuhifadhi Maliasili, TFCG, GFP na wadau wengine kusaidia kutoa elimu.
Akizungumzia changamoto hiyo, Ofisa Misitu wa Wilaya ya Muheza, Obadia Msemo amesema wamekuwa wakichukua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kupanda miti, kutoa elimu ya uhifadhi na kutunza vyanzo vya maji kwa wananchi wote.
Amesema katika msimu wa mwaka 2023 hadi 2024 wamefanikiwa kupanda miti 1,668,000 ambapo zaidi ya miti milioni 1.2 imeweka kukua sawa na asilimia 65 na katika mwaka 2024 hadi 2024 wanatarajia kupata miti milioni 1.5.
“Mabadiliko ya tabianchi katika wilaya yetu tunapambana nayo kwa kuhamasisha upandaji miti, kulima kilimo hifadhi, kutoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kushirikisha makundu yote,” amesema.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here