Home KITAIFA RAIS SAMIA HATAKI MISUKOSUKO KWA WAFANYABIASHARA- DK. BITEKO

RAIS SAMIA HATAKI MISUKOSUKO KWA WAFANYABIASHARA- DK. BITEKO

Google search engine

*Ataka watendaji warasimu wajionee aibu watimize wajibu, watumishi wakumbushwa shughuli za Serikali kufanyika Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
(katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Rafiki Hoteli iliyopo
jijini Dodoma. Kulia kwake ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Adolf Mkenda na kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu na Mmiliki wa
Rafiki Hoteli, Fladmiry Mallya
.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa, Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kama mlezi wa Sekta binafsi nchini na hataki kuona wafanyabiashara  wanapata misukosuko wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema maono ya Rais ni kujenga sekta binafsi itakayokuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la Taifa na ili kufikia azma hiyo, viongozi wengine wahakikishe nia njema ya Rais kwa Wafanyabiashara inatekelezwa kwa vitendo.

Dk. Biteko amesema hayo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Rafiki Hoteli ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (kushoto
mbele) akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Rafiki Hoteli iliyopo
jijini Dodoma.

Aidha, Dk. Biteko amewaagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha wanailea Sekta binafsi na kila mtu atimize wajibu wake kwenye eneo
lake “kama wewe ni Afisa wa TANESCO uliye na wajibu wa kumuunganishia mfanyabiashara umeme ambao mwisho wa siku ataulipia kwa ajili ya mapato yako, huna sababu ya kumwambia njoo kesho wakati kazi hiyo ungeifanya leo.”

Amesema Watendaji ambao ni warasimu lazima waone aibu kwa kuchelewesha shughuli zinazoijenga nchi.

Dk. Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia anataka kuona watanzania wakiwa kwenye daraja la kwanza katika nchi yao na pia waweze kufanya uwekezaji ndani na nje ya nchi bila vikwazo vyovyote.

Kuhusu Sekta ya Utalii nchini, amesema bado kuna changamoto ya upungufu wa vitanda kwa wageni wa ndani na nje ya nchi hivyo bado kuna kazi kubwa ya kuwekeza kwenye sekta ya HIYO ambapo amewapongeza wamiliki wa Rafiki hoteli na wawekezaji wengine ambao
wanaifanyia kazi changamoto hiyo.

Vilevile, Dk. Biteko ameipongeza menejimenti ya hoteli hiyo kwa kutekeleza dhana ya nishati safi ya kupikia kutokana na kuweka
miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye hoteli husika na kutoa wito kwa wananchi kutoharibu mazingira na kutokukata miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesisitiza umuhimu Idara na taasisi mbalimbali Serikalini kutumia miundombinu ya uwekezaji Jijini
Dodoma ambayo ndio Makao Makuu ya Nchi.

Kutokana na hilo ameagiza Watendaji wa Serikali kuhakikisha kwamba shughuli zinazoweza kufanyika ndani ya Mkoa wa Dodoma zifanyike katika Mkoa husika ili pia kutoa fursa kwa wanachi kupata huduma muda wote pale wanapohitaji huduma za watendaji hao.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na Mmiliki wa Rafiki Hoteli Fladmiry Mallya ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji ambayo yanafanya Watanzania kuendelea kuwekeza kwenye nchi yao na hivyo kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kukuza ajira.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here