Home KITAIFA MBUNGE BONNAH ATANGAZA NEEMA KWA WANANCHI UJENZI BARABARA YA LAMI ZIMBILI-KICHANGANI SEGEREA

MBUNGE BONNAH ATANGAZA NEEMA KWA WANANCHI UJENZI BARABARA YA LAMI ZIMBILI-KICHANGANI SEGEREA

Google search engine

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Jimbo la Segerea, wilayani Ilala, Jijini Dar es Salaam, Bonnah Kamoli, amesema dhamira yake ni kuhakikisha barabara katika jimbo hilo zinapitika wakati wote ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa kiwango cha lami, zege au changarawe.

Hayo yameelezwa leo Machi 11,2024 katika hafla ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Ilala kukabidhi mradi wa ujenzi wa barabara ya Zimbili-Kichangani kilomita 0.5 kwa Mkandarasi Kampuni ya SERC Constructions Co. Ltd katika Kata ya Kinyerezi.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge Bonnah, Katibu wa Mbunge, Rutta Rucharaba, amesema ujenzi wa barabara hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na azma ya mbunge huyo kuhakikisha barabara Jimbo la Segerea zinakuwa bora.

Rucharaba amesema, Mbunge Bonnah ana dhamira ya dhati kuondoa changamoto ya barabara katika jimbo hilo kuhakikisha zinapitika wakati wote na zinajengwa kwa viwango na ubora hususan kiwango cha lami, hivyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.

“Pia Mbunge anataka ujenzi wa barabara hii ukamilike kwa wakati na ikiwezekana kabla ya muda. Vilevile Mbunge anataka vijana wa eneo hili wapate ajira katika miradi hii.Kwa sababu hii miradi ni fursa pia ya ajira,”amesema Rucharaba.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kinyerezi, Leah Mgitu, ameipongeza Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Mbunge Bonnah kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kuomba Barabara ya Zimbili- Shule kujengwa kwa kiwango hicho pia.

Wakati huo huo Meneja wa TARURA Ilala, Mhandisi John Magori, amesema, gharama za mradi huo ni Sh. bilioni 1.3 na mradi unatarajiwa kukamilika Septemba 11 mwaka huu na ujenzi tayari umeanza.

Mhandisi huyo, amesema mbali na kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami pia mradi huo utahusisha ukarabati wa Barabara ya Zimbili Kilometa 2.7 kwa kiwango cha changarawe.

Mhandisi wa Kampuni ya SERC, Justine Joseph, amesema watafanya kazi kwa viwango na kukamilisha mradi kwa wakati kwani wana uzoefu wa kutekeleza miradi kama.

Uongozi CCM Kata ya Kinyerezi, umemshukuru Rais Dk. Samia, mbunge, diwani na viongozi wa wilaya na mkoa wa Dar es Salaam, kwa ujenzi wa barabara katika jimbo hilo hususan katika kata hiyo na kuomba ujenzi huo uendelee kwa barabara zaidi hususan zinazopita katika makazi ya watu wengi.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here