Na Faustine Kapama-Mahakama
JAJI Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Hamis Juma, amezindua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na kusisitiza mambo sita kwa wajumbe, ikiwemo kuzingatia maadili na kutunza ziri za ofisi, ambayo yanahitaji kuzingatiwa wanapotekeleza majukumu yao ya kikatiba.
Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi ndogo za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Juma amesema kwa kuzingatia majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo yametajwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4, 2011, watumishi hao wanatakiwa kujituma na kuwa na uwajibikaji wenye tija wakati wa utoaji haki.
Jaji Mkuu pia amesisitiza Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuzingatia kuwa Mahakama ya Tanzania imefanya maboresho ya makusudi kutoka kutumia TEHAMA katika kusambazia taarifa au habari mpaka kuifanya nyenzo muhimu kwenye utendaji kazi wa kila siku wa Mahakama.
“Maboresho yanayoendelea ndani ya Mahakama yawe chachu kwa Sekreterieti ya Tume kuwezesha kazi zake na za Tume ziweze kutumia TEHAMA katika shughuli zao za kila siku, mfano utunzaji wa kumbukumbu na taarifa na kwenye mikutano ya Tume na Kamati zake ili zipunguze na kuondoa kabisa matumizi ya karatasi,” amesisitiza.
Aidha, Jaji Mkuu amewahimiza watumishi wa Sekreterieti kuwa wabunifu (creativity, innovative) katika kazi zao za kuiwezesha Tume ya Utumishi kutimiza wajibu wake wa kikatiba na kisheria. Amesema ubunifu ni lazima ujengwe kutokana na misingi imara ya uelewa wa kina wa vifungu vya Katiba, sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayoongoza Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Ubunifu unaongezwa kwa kujisomea, kujitafutia taarifa na kujiboresha kwa kujifunza kutoka Tume zingine za Mahakama zenye viwango vya ubora,” Prof. Juma amebainisha. Kadhalika, Jaji Mkuu alisisitiza suala la maadili mema.
Amesema Tume ya Utumishi wa Mahakama imepewa jukumu la kikatiba la kusimamia maadili na nidhamu, hivyo wafanyakazi wa Sekreterieti ya Tume wanatakiwa kuwa na maadili yasiyotiliwa shaka. Jaji Mkuu amesema itakuwa kichekesho kwa Tume kuhubiri maadili huku watumishi katika Sekretarieti wakikosa uadilifu wanapotekeleza majukumu yao.
Jambo jingine ambalo Mhe. Prof. Juma amesisitiza linahusu utunzaji wa siri za ofisi. Amesema Sheria ya Usimamizi wa Mahakama, Na. 4/2011 imesheheni vifungu kadhaa ambavyo vinasisitiza umuhimu wa kutunza siri za ofisi.
“Kifungu cha 16 (1) cha Sheria hii, kinahusu wajibu wa Makamishna, Katibu na Naibu Katibu kuapa mbele ya Mwenyekiti kabla ya kuanza shughuli za Tume. Kifungu kidogo cha (2) kimempa Mwenyekiti mamlaka ya kumtaka mtumishi yoyote katika Sekreterieti ya Tume, kula kiapo kwa mujibu wa Jedwali la Tatu la Sheria Na. 4/2011,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa msisitizo wa vifungu vya sheria ni kumbusho kwa watumishi kuwa ni kinyume cha sheria kwa mtumishi wa Tume kutoa taarifa yoyote ya Tume kwa mtu asiyehusika bila kibali ama kuzingatia taratibu. Aidha, aliweka mkazo katika suala zima la utii wa kazi, kwa viongozi na pia kuheshimiana.
“Haya yote yakizingatiwa utendaji utakuwa wenye tija. Chukueni tahadhari zote kila wakati kwa kuwa ndugu, majirani na marafiki watakaposikia kuwa wewe upo Sekretarieti ya Tume watakutafuta ili uwashauri. Epukeni mtego huo kwa kuwa kufanya hivyo ni ukiukaji wa maadili. Kwa muktadha huo, upo umuhimu wa viapo kushushwa kwa watumishi wote wa Sekretarieti,” amesema.
Awali akimkaribisha kuzindua Baraza hilo, Prof. Ole Gabriel alimweleza Jaji Mkuu kuwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, watumishi wa Sekretarieti ya Tume huongozwa na Dira ya Tume ambayo ni kuwa kitovu cha ubora katika kusimamia watumishi wa Mahakama Tanzania Bara. Aidha, alisema watumishi hao wanaongozwa na Dhima ya Tume ambayo ni utoaji endelevu wa huduma ya ushauri na usimamizi wa rasilimali watu katika utumishi wa Mahakama Tanzania Bara.
Mtendaji Mkuu alieleza pia kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Sekretarieti ya Tume imejiwekea malengo ambayo yatasaidia kufanikisha majukumu yake, ikiwemo uwezeshaji wa maadili katika Mahakama ya Tanzania unaboreshwa na kuimarisha huduma za utawala bora katika Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Kwa hiyo, kimsingi tunajitahidi kuhakikisha kuwa utawala bora unakuwepo na pia mpango mkakati wa kuzuia rushwa unatekelezwa kwa ufanisi. Kama mnavyofahamu katika shughuli za watumishi wa Mahakama masuala ya maadili na kupambana na rushwa ni jambo la msingi sana,” alisema.
Prof. Ole Gabriel alieleza pia kuwa katika kipindi cha Julai 2022 hadi Disemba 2022 Sekretarieti ya Tume imefanikiwa kutekeleza majukukumu yake, ikiwemo kuwezesha Tume kufanya vikao vitatu na katika masuala mbalimbali kama uteuzi wa Majaji 22 wa Mahakama Kuu na Msajili wa Mahakama ya Rufani, kuthibishwa kwenye uongozi na ajira katika masharti ya kudumu kwa baadhi ya watumishi na kusimamia nidhamu na maadili.