* WALOWEZI WALIOJIORODHESHA SASA WAFIKIA 11,037, WENGINE WATAKIWA KUJITOKEZA KABLA YA MSAKO
Na MWANDISHI WETU
-MTWARA
KATIKA kuhakikisha kauli mbiu ya tunaifungua Mtwara inatekelezeka, Idara ya Uhamiaji imefungua mipaka ya Kilambo na Mkunya ili kuwezesha watu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine
Kauli hiyo imetolewa leo, Machi 16, 2024 na Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara (ACID) Dismas Mosha wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kwenye jengo jipya la Uhamiaji lililopo Manispaa ya Mtwara Mikindani
Amesema mipaka hiyo ilifungwa kwa muda ila kwa sasa imeshafunguliwa ili kuifungua Mtwara na watu waweze kutoka nje kutafuta fursa za biashara na za maendeleo, sambamba na hilo amesema wanaendelea kutoa elimu kwa umma katika ngazi zote kuanzia shule, vijiji na kata lengo ni kusisitiza usalama wa nchi
“Tunatoa elimu kwa umma na muitikio ni mkubwa, lengo ni kusisitiza usalama wa nchi maana ulinzi wa nchi yetu ni wa kila mwananchi wa Tanzani, na hasa mzalendo kama Katiba inavyotuambia, tuna kauli mbiu yetu ya ‘mjue jirani yako’, hii ni kwa ajili ya usalama wetu sisi wenyewe na hii kauli imeitikiwa na watu wote,” amesema ACID Mosha
Kutokana na hali hiyo, amesema kuwa sababu kubwa ya kufunga mipaka hiyo ni vurugu zilizokuwa zinaendelea upande wa nchi jirani (Msumbiji) hivyo ni ngumu kumtoa mtu upande wa Tanzania kumpeleka nchi jirani wakati kuna machafuko
“Tuliahirisha shughuli zetu kwa sababu upande wa pili kulikuwa na vurugu, unavyomuhudumia mtu kutoka nje ya nchi unatakiwa aende kule ahudumiwe na serikali iliyopo, sasa upande wa pili kulikuwa na machafuko hivyo huwezi kumtoa mtu wako aende kule kwa ajili ya biashara wakati kule hakuna mtu wa kumuhudumia, Passport yetu imeandikwa kabisa Rais wa nchi anaomba mtu wangu achungwe, alindwe,” amesema
Ameongeza kuwa hadi sasa walowezi waliojiorodhesha ni 11,037 huku akiwaomba wajitokeze kujiandikisha ili waweze kuwa sehemu ya Tanzania na kuacha kukaa kwa mashaka
Sambamba na hilo amesema toka mipaka hiyo ifunguliwe kwa sasa uingiaji na utokaji wa wananchi ni mkubwa katika mpaka wa Kilambo, Mkunya pamoja na Mtambaswala.
UTUNZAJI MAZINGIRA
Wananchi mkoani Mtwara wamepewa rai ya kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kupata hewa safi na kuepuka matumizi ya kuni ambayo sio sahihi
Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara (ACID) Dismas Mosha, ametoa kauli hiyo kwenye zoezi la upandaji miti lililoongozwa na idara ya uhamiaji kwenye jengo lao jipya lililopo Manispaa ya Mtwara Mikindani
Amesema wanaungana na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanaboresha mazingira ili yawe mazuri kwa vizazi vya sasa na vijavyo, sambamba na kutoa wito kwa jamii kutunza mazingira na kuepuka matumizi ambayo sio sahihi badala yake watumie nishati mbadala kwa ajili ya kulinda mazingira ili kukwepa hewa ya ukaa
“Mazingira ndio kila kitu, tutunze mazingira na yenyewe yatutunze kwa kupanda miti na kukwepa hasa yale matumizi ambayo sio sahihi sana ya nishati ya kuni na tutafute nishati mbadala ya gesi kwa ajili ya kulinda mazingira yetu, pia tukwepe ile hewa ya uka,” amesema ACID Mosha