Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Mamlaka hiyo, Johansen Kahatano amesema LATRA ilifuatilia Mfumo wa ufuatiliaji mwenendo wa Magari (VTS) na kukuta vifaa vyake vinafanya kazi vizuri katika Gari aina ya ‘Coaster’ ambayo iligongana na Lori aina ya Mitsubishi Fuso kwenye ajali iliyotokea eneo la Magila, wilayani Korogwe na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 12 kujeruhiwa.
“Katika ajali iliyotolea kule Korogwe, Gari aina ya ‘Coaster’ (Special Hire) iliyokuwa inapeleka msiba Moshi mkoani Kilimanjaro, tulifuatilia mfumo wa taarifa wa ufuatiliaji mwenendo na tulibaini, Gari ya mizigo (Lori) lilikuwa limebeba Ndizi lilikuwa kwenye spidi kubwa, kwenye ‘kona’ lakini pia ilitaka kupita Gari nyingine,” amesema Kahatano.
“Kutokana na spidi ya Lori kuwa kubwa, huyu mwenye ‘Coaster’ alijitahidi lakini alishindwa kumkwepa mwenye Lori na hivyo kusababisha ajali. Sisi tulithibitisha kwa umbali ambao ‘Coaster’ ilirudi nyuma kwa zaidi ya mita 32 baada ya kupigwa na Lori lile ambalo lilikuwa kwenye spidi kubwa,” ameeleza Kahatano.
Aidha, Kahatano ametoa ufafanuzi wa ajali iliyotokea wilayani Kongwa mkoani Dodoma ambayo ilihusisha Basi kubwa la Kampuni ya Frester na Gari kubwa aina ya Lori (Scania) na kusababisha vifo vya watu 12 na wengine 63 kujeruhiwa.
“Dereva wa Basi kubwa hakuwa kwenye spidi kubwa lakini alikosea alitaka kupita gari nyingine, ghafla Gari nyingine ikawa inakuja mbele yake, Gari analolipita likawa limesimama akataka kumpisha mwenye Lori (Scania), wakawa wanapishana sasa wakakutana huko huko nje ya Barabara na kusababisha ajali hiyo,” amesema Kahatano.