Home KITAIFA DK. BITEKO ASHIRIKI SHEREHE ZA KUWEKWA WAKFU NA KUSIMIKWA ASKOFU MPYA JIMBO...

DK. BITEKO ASHIRIKI SHEREHE ZA KUWEKWA WAKFU NA KUSIMIKWA ASKOFU MPYA JIMBO KATOLIKI LA MAFINGA

Google search engine

*ASEMA RAIS SAMIA ANAENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KWA MADHEHEBU YA DINI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto  Biteko (kulia) akimpongeza Askofu Mpya wa Jimbo jipya  Katoliki la Mafinga, Mhashamu Vincent Cosmas Mwagala mara baada ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu huyo Mpya wilayani Mufindi mkoani Iringa

Na MWANDISHI WETU

-IRINGA

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dk. Doto  Biteko amemwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo jipya Katoliki la Mafinga, Mhashamu Vincent Cosmas Mwagala na kueleza kuwa Dk. Samia anaendelea kutoa  kila aina ya ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhahebu mengine ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

Amesema, nia ya Rais, Dkt. Samia ni kuona wananchi wanapata huduma bora katika nyanja mbalimbali ikiwemo Zahanati, Barabara, Maji, Shule na Umeme wa uhakika hivyo ili kutekeleza suala hilo kwa ufanisi Serikali inashirikiana na Taasisi binafsi ikiwemo madhehebu mbalimbali ya dini katika kuwapelekea maendeleo wananchi. n.k

Akizungumza na wananchi waliohudhuria sherehe hiyo katika Halmashauri ya Mafinga, Wilayani Mufindi  mkoani Iringa, Dk. Biteko amesisitiza kuhusu utunzaji wa mazingira na kutoa angalizo kuwa yeyote anayeharibu mazingira lazima aonekane kama adui na achukuliwe hatua kwani athari za kutokutunza mazingira ni kubwa, akitolea mfano kuwepo kwa mgawo wa umeme kutokana na kutokuwa na maji ya kutosha kuzalisha umeme.

“Leo tumejenga mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere, mradi ule ni mkubwa sana, lile si bwawa tu bali ni ziwa kwani urefu wake ni kilometa 100 na upana wake ni kilometa 25, uwepo wake unahitaji maji na ikizingatiwa kuwa gharama nyingi zimetumika kujenga mradi huo zaidi  ya Shilingi Trilioni Sita, ni  lazima tulinde mazingira ili kupata faida mbalimbali ikiwemo maji ya kutosha kuzalisha umeme,” amesema Dk. Biteko

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema kuwa  Machi 19, 2024, Rais, Dk. Samia ametimiza miaka mitatu akiwa madarakani ambapo amedhihirisha kwa vitendo kuwa ni kiongozi bora ambaye  ameendelea kuiweka nchi katika hali ya utulivu.

Ameongeza kuwa, Rais, Dk. Samia ameendelea kutekeleza miradi mbalimbali aliyoikuta mara baada ya kuapishwa ikiwemo barabara, reli, umeme na ameendelea kubuni miradi mipya na kuiendeleza kwa kasi kubwa.

Dk. Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Dini na Watanzania kumuombe Rais Samia ili aendelee kuongoza nchi kwa ufanisi akiwa na afya njema na pia kuiombea nchi ili iendelee kuwa ni mahali salama pa kuishi.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dk. Biteko ametoa wito kwa Watanzania  kuchagua viongozi wanaokerwa na shida za wananchi na wanaozitatua na kwamba wasichague viongozi kwa kigezo cha ukabila, dini au mahali walipotoka bali msingi uwe ni maendeleo na utanzania.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dk. Doto  Biteko (katikati) na viongozi wengine wakiwa katika Sherehe ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo jipya Katoliki la Mafinga, Mhashamu Vincent Cosmas Mwagala zilizofanyika Halmashauri ya Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa. Wa Pili kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile .Watatu kushoto ni  Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba na wa pili kulia ni Spika Mstaafu, Mama Anna Makinda.

Kwa upande wake, Askofu Mpya wa Jimbo la Mafinga, Mhashamu Vincent Mwagala amesema Kanisa Katoliki litaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika masuala ya ya ustawi wa jamii ili amani iendelee kutamalaki na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Pia amemshukuru Dk. Biteko kwa kuhudhuria sherehe hiyo na kuwasilisha ujumbe wenye matashi mema kutoka kwa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile na  Spika Mstaafu, Mama Anna Makinda.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here