Home KITAIFA RC MWASSA APIGIA CHAPUO ULINZI WA MAZINGIRA ZIWA VICTORIA

RC MWASSA APIGIA CHAPUO ULINZI WA MAZINGIRA ZIWA VICTORIA

Google search engine
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa akifungua mafunzo ya namna namna ya utunzaji mazingira katika Ziwa Victoria hasa katika kuepuka umwagaji mafuta kama njia ya kulinda maziwa na bahari

Na MWANDISHI WETU

-KAGERA

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa amewataka wananchi na wadau wa usafirishaji wanaofanya shughuli ndani ya Ziwa Victoria, kutofanya mambo yanayoweza kuathiri na kusababisha uchafuzi wa mazingira katika ziwa hilo kama mkakati wa kuendana na mpango wa Taifa wa kupambana na vitendo hivyo ikiwemo umwagikaji wa mafuta kwenye ziwa na bahari

Hayo ameyasema wakati wa warsha ya mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Kagera Machi 20, 2024 yenye lengo la kudhibiti vitendo vya umwagikaji mafuta ndani ya Ziwa Victoria.

Kutokana na hali hiyo RC Mwassa amesema kuwa mafunzo haya yana umuhimu mkubwa kwa eneo la Mkoa Kagera kwa kuwa pia Ziwa Victoria linagusa Wilaya za Mkoa Kagera, hivyo utunzaji wa ziwa hilo unagusa jamii yetu kwa kuwa maji hayo hutumika katika shughuli nyingine za kibinadamu.

Mwassa amesisitiza kuwa shughuli nyingine za uvuvi zimekuwa zikifanyika humo, hivyo endapo vitendo vya umwagaji mafuta katika ziwa havitakomeshwa na wala kuchukuliwa hatua za kupambana navyo, itapelekea kukosekana kwa mazao ya samaki  ambao pia hutumiwa kama kitoweo.

“Ikiwatutaacha hili, litaathiri upatikanaji wa samaki bora, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa pato la mtu mmoja mmoja (mvuvi) na Pato la Taifa,  kwa mfano kwa Wilaya ya Muleba ambayo kwa asilimia kubwa mapato ya Halmashauri hiyo hutegema shughuli za uvuvi hasa dagaa,” amesema Rc Mwassa

Hata hivyo Mwassa amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri wa mapambano hayo na kuwa yale watakayofundishwa na kujifunza yakawe chachu ya kuendelea kudhibiti na kukomesha pamoja na kushughulikia matendo kama hayo ya uchafuzi na umwagaji mafuta ziwani pale yatakapojitokeza.

Mafunzo hayo muhimu kwa maslahi ya Taifa, ambayo ni mpango wa kitaifa wa kudhibiti uchafuzi wa maziwa na bahari kwa umwagaji wa mafuta yamekuja wakati ambapo nchi za jirani Uganda na Kenya wapo katika mchakato wa hatua za uchimbaji wa mafuta ziwani ambapo shughuli ikikamilika ya uchimbaji mafuta hayo yatasafirishwa kupitia Ziwa Victoria.

Mafunzo hayo yamewashirikisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na shughuli za ziwani kwa kupata elimu ya nadharia na kisha kupata elimu ya vitendo kutoka kwa Watumishi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),  huku wengi wao wakionekana kufurahishwa na jinsi mafunzo yalivyoratibiwa na wawezeshaji hao.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here