* UCHUMI WAZIDI KUPAA HIVI SASA WAFIKIA ASILIMIA 5.2
Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
NI mfanikio lukuki ndivyo unaweza kusema. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Saia Suluhu Hassan, imefanikiwa kukuza Pato la Taifa kupitia sekta mbalimbali ikiwamo ya utalii nchini.
Kutokana na hali hiyo imeelezwa kuwa Sekta inayoongoza hivi sasa kwa kuiletea nchi fedha za kigeni ambapo sasa zimefikia dola za Marekani bilioni 3.37 (zaidi ya shilingi trilioni 8) ni sekta ya utalii.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan madarani, Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi, amesema kuwa sekta hiyo imemrejeshea shukurani mkuu huyo wa nchi kutokana na juhudi zake binafsi za kutoka ofisini na kwenda kushiriki katika utengenezaji wa filamu ya “Tanzania: The Royal Tour”.
Matinyi, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi mapato dola za Marekani bilioni 1.31 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza dola bilioni 3.37.
“Kwa kuongeza idadi ya watalii wengi baada ya mlipuko wa UVIKO-19 Tanzania sasa inashika nafasi ya pili barani Afrika baada ya Ethiopia; na kwa kuongeza mapato makubwa inashika nafasi ya tatu baada ya Moroko na Morisi (Mauritius).
“Tanzania imeendelea kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali. Tuzo hizo ni Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, Tanzania kuwa nchi ya saba miongoni mwa nchi 18 duniani zilizo bora kutembelewa kiutalii kwa mwaka 2022, Hifadhi ya Taifa Serengeti kumeorodheshwa kama eneo maridhawa la kutembelewa kwa mwaka 2023 na Hifadhi ya Taifa Serengeti kushika nafasi ya tatu ya vivutio bora vya asili duniani kwa mwaka 2023,” amesema Matinyi
Aidha, amesema kuwa Mamlaka ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imeshinda tuzo mbili za Best of the Best Travelers’ Choice na Africa’s Leading Tourist Destination kwa mwaka 2023, mazo ni baadhi ya tuzo ambazo Tanzania imezipata kimataifa.
UCHUMI, FEDHA NA UWEKEZAJI
Akizungumzia maeneleo ya kiuchumi Msemaji huyo wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, amesema kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mlipuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita za Urusi na Ukraine na pia huko Mashariki ya Kati.
Amesema matatizo hayo yaliutikisa uchumi wa Tanzania uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia 7 na kuushusha hadi asilimia 4.2 mwaka 2020.
Hata Matinyi, amesema kuwa hivi sasa ukuaji umefikia asilimia 5.2 kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita.
“Aidha, Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila mwananchi kwa mwaka (GNI per capita) ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080, lakini mwaka 2022 ni dola 1,200.
“Serikali pia imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya asilimia 4- kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“…vile vile, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi Desemba 2023, nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.5, ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4. Akiba hiyo ni sawa na dola za Marekani bilioni 5.4,” amesema
UKUSANYAJI MAPATO
Amesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri katika kipindi cha miaka mitatu hii kwa kufuata mwongozo wa Rais wa kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara na kujali changamoto wakati wa kukusanya kodi.
“Hivyo basi, makusanyo yamefikia shilingi 2 trilioni 24.14 kwa mwaka 2022/23 kutoka shilingi trilioni 18.15 mwaka 2020/21. Hili ni ongezeko la shilingi trilioni 5.99.
“Aidha, kwa mwezi Desemba 2023, TRA ilivunja rekodi ya ukusanyaji ya kila mwezi baada ya kufanikiwa kukusanya shilingi trilioni 3.05 licha ya kuwa wastani kwa mwaka huu hadi sasa ni shilingi trilioni 2.13. Ni vema kufahamu kwamba hadi kufikia Machi 20, 2024, TRA ilikuwa imeshakusanya kiasi cha shilingi trilioni 19.21, ikiwa ni dalili mkwamba itavuka kiasi cha mwaka uliopita,” amesema Matinyi
UWEKEZAJI
Akieleza kuhusu suala la uwekezaji katika kipindi mwaka Machi 2021 hadi Machi 2024, Msemaji huyo wa Serikali aesema kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefanikiwa kusajili jumla ya miradi 1,188 ambayo ilikadiriwa kuwekeza kiasi cha mtaji wa dola za Marekani milioni 15,041 na kutoa jumla ya ajira 345,464.
Amesema kati ya miradi hiyo asilimia 35 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 41 ni ya wageni na asilimia 24 ni ya ubia kati ya Watanzania na wageni.
Aidha, amesema kuwa Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uwekezaji (National Investment Steering Committee– NISC) ilitoa idhini ya kusainiwa mikataba ya utekelezaji kwa miradi 16.
“Miradi hiyo yenye hadhi ya mirahi mahiri ni pamoja na Mradi wa Bagamoyo Sugar Limited; Mradi wa Kagera Sugar Limited; na Mradi wa Mtibwa Sugar Estate Limited;.
Vile vile, NISC iliridhia miradi mingine nane ambayo ilisaini mikataba ya utekelezaji na TIC, yaani (perfomance contracts) baada ya kupewa hadhi ya kuwa wawekezaji mahiri maalum.
“Katika kundi hili kuna wa upanuzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari wa Kampuni ya Kilombero Sugar Limited; na pia Mradi wa kilimo cha miwa na kiwanda cha kuzalisha sukari wa Kampuni ya Mufindi Paper Mills Limited – Kasulu,”amesema
OFISI YA MSAJILI WA HAZINA
Matinyi, amesema kuwa thamani ya uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongezeka kutoka shilingi trilioni 70 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 76 mwaka 2023 – sawa na ongezeko la asilimia 8.6.
Ametaja sababu ya ongezeko hilo kuwa ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa.
Aidha amesema kuwa ofisi pia imeongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kutoka shilingi bilioni 637.66 hadi trilioni 1.008 kwa mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 58.
“Serikali pia imeongeza umiliki wa hisa katika kampuni ya almasi ya Williamson Diamonds kutoka asilimia 25 hadi 37 huku ikisaini mikataba ya ubia wa asilimia 16 zisizohamishika katika kampuni za madini,” amesema
SEKTA YA MADINI
Amesemakatika kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2024 Wizara ya Madini imefanikiwa kuiendeleza sekta kwa namna mbalimbali ikiwemo kukusanya maduhuli yatokanayo na ada mbalimbali, mirabaha, faini na penati na kufikisha kiasi cha Shilingi trilioni 1.93.
Amesema awali mwaka 2021/22 ilikuwa shilingi bilioni 591.5 lakini hadi kufikia mwaka 2023/24 imefikia shilingi bilioni 690.4.
“Aidha, katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022 mauzo ya madini mbalimbali yalikuwa shilingi bilioni 157.34 lakini kufikia kipindi cha Machi 2023 hadi Februari 2024 mauzo yamefikia shilingi bilioni 476.8,” amesema
KILIMO
Matinyi, amesma kuwa bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294.16 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni shilingi bilioni 970.78 mwaka wa fedha 2023/2024.
Matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 320,233 kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tani 580,628 kwa mwaka wa fedha 2022/23.
“Bajeti ya maendeleo ya umwagiliaji imeongezeka kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 361.5 mwaka 2023/24 ambapo wataalam wa kilimo 320 wameajiriwa na kusambazwa katika ofisi za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 139. Mitambo 15 na magari 53 vimenunuliwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji.
“Eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 694,715 mwaka 2020/2021 hadi hekta 727,280.6 mwaka 2022/2023,” amesema
Aidha, ameema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji zenye hekta 95,000 zilizoanza mwaka 2022/2023 pamoja na kuanza skimu mpya zenye ukubwa hekta 95,000 kwa mwaka 2023/2024, ambapo kukamilika kwake kutaongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 917,280.
“Programu ya Vijana ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Build Better Tomorrow-BBT). Mradi unashirikisha vijana 688, ambao wameanza kilimo biashara katika shamba la Chinangali II,” amesema
UFUGAJI NA UVUVI
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu 2021/22 hadi mwaka 2023/24, bajeti ya sekta ya mifugo imekua ikiongezeka kwa kasi, ambapo bajeti hiyo imeongezeka kutoka shilingi 47,844,950,000/- mwaka 2021/22 hadi shilingi 112,046,777,000/- mwaka 2023/24.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu, 2021/22 hadi mwaka 2023/24, bajeti ya sekta ya uvuvi imepanda kutoka shilingi 121,350,046,999/- mwaka 2021/22 hadi shilingi 183,874,156,000 mwaka 2023/24.
“Ili kuhakikisha Serikali inarasimisha shughuli za uvuvi, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Januari 30, 2024, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, alizindua zoezi la ugawaji wa boti 160 na vizimba 222, kwa ajili ya makampuni, watu binafsi na vikundi vya wavuvi kupata vitendea kazi hivyo kwa njia ya mkopo usio na riba. Sasa bandari ya uvuvi inajengwa Kilwa Masoko,” amesema
MIUNDOMBINU NA UCHUKUZI
Kuhusu Reli ya Kisasa (SGR), Matinyi amesema kuwa itakumbukwa kwamba mara alipoingia madarakani, Rais Samia aliahidi kumalizia ujenzi wa vipande vilivyoanzishwa na awamu ya tano sambamba na kuanza kwa ujenzi kwa vipande vya Makutupora-Tabora (km 368), Tabora-Isaka (km 165), Isaka-Mwanza (km 341) na TaboraKigoma (km 506).
“Wakati huo kipande cha Dar es Salaam-Morogoro kilikuwa kimefikia 83.55% na cha Morogoro-Makatupora 57.57% vikiwa na jumla ya kilomita 722. Hadi sasa utekelezaji umefikia 98.90% kwa kipande cha kwanza na asilimia 96.51 kwa kipande cha pili. Tayari fedha zimeshalipwa kiasi cha shilingi trilioni 6.805 kati ya shilingi trilioni 7.4 zilizotakiwa.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dk. Samia Suluhu Hassan ilianzisha ujenzi wa vipande vitano vipya ambapo vitatu ni katika kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Mwanza, yaani Makutupora hadi Tabora (km 368) ambapo ujenzi umefikia asilimia 13.98, Tabora hadi Isaka (km165) sasa ujenzi umefikia 5.44%; na Isaka hadi Mwanza (km341) ambapo ujenzi umefikia 31.07,” amesema
Aidha, amesema kuwa ujenzi wa awamu ya pili umeanza kwa vipande vya Tabora hadi Kigoma (km506) na kwa Uvinza hadi Musongati (km367) hivi sasa taratibu za ununuzi zinaendelea. Hii inafanya jumla ya kilomita 1,560 za ujenzi wa SGR kutekelezwa ndani ya serikali ya awamu ya sita -sawa na asilimia 68.4 ya ujenzi unaoendelea.
Matinyi, amesema kuwa thamani ya uwekezaji huu imefikia trilioni 23.3 ukiondoa kipande cha Uvinza hadi Musongati ambacho kipo katika hatua ya ununuzi.
“Jumla ya shilingi trilioni 10.1 zimeshalipwa kwa wakandarasi kwa mujibu wa hati za malipo na malipo ya awali kwa vipande vipya.
“Serikali pia inafanya ununuzi wa treni za kisasa (EMU) seti 10; mabehewa ya abiria 89; na mabehewa ya mizigo 1,430. Uwekezaji huu una thamani ya dola za Marekani milioni 508.6 – sawa na shilingi trilioni 1.2,” amesema
Msemaji huyo wa Serikali, amesema kuwa Rais Samia alishatoa maelekezo kuhakikisha reli hii mpya inayafikia masoko ya kikanda kwa nchi jirani ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi na DRC ili kuleta manufaa makubwa. Juhudi zinaendelea na makubaliano na nchi hizi yameshafikiwa ili reli itoke Uvinza, Tanzania, iende hadi Kindu nchini DRC kupitia Musongati-Gitega-Bujumbura nchini Burundi.
BANDARI
Kuhusu Bnadari, amesema kuwa meli ziliongezeka kutoka 4,318 Machi 2021 hadi kufikia meli 4,762 Februari 2024, sawa na ongezeko la asilimia 10.28. Kiwango hiki cha ukuaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 11.79 kwa mwaka.
Amesema shehena iliyohudumiwa iliongezeka kutoka tani milioni 17.287 Machi 2021 hadi kufikia tani milioni 26.544 Februari 2024, sawa na ongezeko la asilimia 37.9. Kiwango hiki cha ukuaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 15.4 kwa mwaka.
“Shehena za makasha na shehena za magari ziliongezeka. Shehena ya nchi jirani iliongezeka kutoka tani 6,166,052 Machi 2021 hadi kufikia tani 9,452,535 Februari 2024, sawa na ongezeko la asilimia 53.3. Kiwango hiki cha ukuaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 26.5 kwa mwaka.
“Katika kipindi cha Awamu ya Sita, Serikali imeweza kukamilisha yafuatayo; ujenzi wa gati maalumu la kuhudumia meli za magari (Gati Na. 0), uboreshaji wa gati Na. 1 – 4 kwa ajili ya kuhudumia shehena mchanganyiko, gati Na 5 – 7 kwa ajili ya kuhudumia shehena ya makasha,
“Kuongeza kina cha gati 1-7 kutoka mita 11 hadi kufikia mita 14.5, na kukamilika kwa ujenzi wa yadi ya kuhudumia makasha, kuchimba na kupanua lango la kuingilia meli na sehemu ya kugeuzia meli,” amesema
Amesema mbali ya Serikali kuongeza vifaa vya kisasa, lakini pia kuna upanuzi wa bandari za Tanga, Mtwara, na zile za maziwa ili kukidhi mahitaji ya soko katika nchi jirani ambayo yanaongezeka siku hadi.
USAFIRI WA ANGA
Kuhusu sekta ya usafiri wa anga, amesema kuwa Serikali iliendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuwekeza zaidi ikiwemo kununua ndege ili kulifanya limudu kutoa huduma na kuchochea ukuaji wa sekta ingine za kiuchumi.
Amesema katika miaka mitatu Serikali imenunua ndege tano zikiwemo tatu za masafa ya kati ambazo ni Airbus A220 mbili; Boeing 737 Max9; Boeing 767-300F ya mizigo na Dash 8 Q-400 na zote zinaendelea kutoa huduma.
“Ndege mbili zaidi, Boeing 737 Max9 (iko katika hatua ya makabidhiano) na moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 (katika hatua ya uundwaji) tayari zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kuwasili nchini mwezi Machi na Aprili mwaka huu.
“Hivyo basi, kwa kujumuisha na uwekezaji huu sasa ATCL ina jumla ya ndege za abiria 12 na moja ya mizigo zinazohuduma vituo 24 kutoka vituo 19 vya mwaka 2021 na inatarajiwa vitaongezeka.
“Kwa ujumla wake, ATCL imeongeza abiria kutoka 537,155 mwaka 2021 hadi 1,070,734; tani za mizigo 1,290 mwaka 2021 hadi 3,561; na miruko 10,550 mwaka 2021 hadi 17,198 mwaka 2023,” amesema
UJENZI WA BARABARA
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu (2021 -2024), Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imefanikiwa kukamilisha miradi 25 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,198.50. Katika kipindi hicho, jumla ya barabara 57 zenye urefu wa kilometa 3, 794.1 ziko hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Kadhalika, miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa nane imekamilika. Aidha, miradi mitano ya ujenzi wa madaraja inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kielelezo wa ujenzi wa daraja la J. P. Magufuli (Kigongo – Busisi) mkoani Mwanza lenye urefu wa mita 3,200 kwenye Ziwa Victoria
“Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza miradi ya viwanja vya ndege ambapo vitano vimekamilika, miradi nane inaendelea chini ya TANROADS. Miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege inayoendelea ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, ambacho kinajengwa kwa fedha za Serikali (GOT) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),” amesema
BARABARA MIJINI NA VIJIJINI
Matinyi, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti ya uboreshaji miundombinu chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na kufikia jumla ya shilingi trilioni 2.53 katika kipindi cha miaka mitatu.
Amesema fedha hizo zimewezesha ujenzi wa barabara za lami za kilomita 819.22 (tofauti na barabara za lami zilizo chini ya TANROADS) na hivyo kuongeza mtandao wake kutoka kilomita 2,404.90 hadi 3,224.12.
“Kwa upande wa barabara za changarawe, jumla ya kilomita 11,924.36 zimejengwa na kuongeza mtandao wake kutoka kilomita 29,183.36 hadi 41,107.52. Kumekuwa pia na ujenzi wa madaraja mengi nchini ikiwemo kutumia teknolojia ya mawe.
“Aidha, TARURA imepokea wito wa Mheshimiwa Rais wa kuhakikisha sasa inatumia teknolojia mbadala ambapo majaribio ya teknolojia ya ECOROADS yameonesha mafanikio makubwa ambapo kilomita 22 zilijengwa katika eneo korofi na teknolojia hii kuhimili changamoto za eneo hilo,” amesema
UZALISHAJI UMEME
Amesema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kihistoria wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji kwenye bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP). Mradi huo utakuwa na vinu tisa vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 235 kila kimoja na kufanya jumla ya megawati 2,115.
“Ikumbukwe kwamba uwezo wa jumla wa kuzalisha umeme katika nchi yetu hivi sasa ni megawati 1,911 tu. Wakati Rais Dk. Samia anaingia madarakani, ujenzi wa bwawa hili ulikuwa umefikia asilimia 33 lakini hivi sasa umekamilika kwaasilimia 96.28. Kinu Na. 9 kimeshawashwa na Na. 8 kinatarajiwa kuwashwa mwezi huu kikifuatiwa karibuni na kinu Na. 7. Mradi huu mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unagharimu shilingi trilioni 6.5 na mpaka sasa serikali imeshamlipa mkandarasi shilingi trilioni 5.7 – sawa na asilimia 88.7,” amesema
Miradi mingine ni ya ujenzi wa njia kubwa za kusafirisha umeme ambazo zitaunganisha mikoa mbalimbali hadi nchi jirani ambapo kutaiwezesha Tanzania kuuza nishati hiyo nje ya nchi pindi itapozalisha umeme wa ziada.
Ameitaja nchi hizo ni Uganda; Kenya itakayounganisha hadi Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan na Misri pamoja na Zambia itakayounganisha umeme wa Tanzania na wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, chini ya TANESCO miradi ya vyanzo vingine inafanyiwa kazi ili hatimaye Tanzania ifikie uzalishaji wa megawati 10,000 ifikapo mwaka 2035.
UMEME VIJIJINI
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeunganisha jumla ya vijiji 5,481 na kufikisha vijiji vyenye kuwa 11,843 – sawa na 96.14% ya vijiji vyote nchini ambavyo ni 12,318.
Vile vile, vitongoji 5,562 vimefikishiwa huduma ya umeme na kufanya jumla kuwa vitongoji 32,750 (51%) ya vitongoji vyote nchini ambavyo ni 64,760. Inatarajiwa kwamba kabla ya mwaka 2025 kumalizika, vitongoji vingine 8,150 vitakuwa vimefikishiwa umeme.