Na MWANDISHI WETU
-MWANZA
KAMATI ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), wameipongeza TARURA kwa kudhibiti ongezeko la gharama ya mikataba ya ujenzi wa barabara za wilaya nchini
Hayo yamesemwa leo Machi 25, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), Japheti Hasunga na wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara za Buhongwa-Bulale na Luchelele zilizojengwa kwa kiwango cha lami katika Halmashauti ya Nyamagana Jijini Mwanza.
Kamati hiyo wameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa usimamizi mzuri wa Mikataba ya Ujenzi wa Barabara za Wilaya uliopelekea kutokuongezeka kwa gharama za Mikataba iliyosainiwa na Makandarasi.
Hasunga amesema kamati yao imeridhishwa na utendaji kazi wa wataalam wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na TARURA kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, PAC imeishauri TARURA kuzingatia ujenzi wa vivuko vidogo vya watembea kwa miguu katika mifereji ya barabara kwa ajili ya usalama wa watumiaji hasa kwenye maeneo ya makazi pamoja na kuchora mistari ya alama (Zebra) kwa ajili ya usalama wa wavukaji wa barabara kwa miguu.
Pia imesisitiza usanifu wa barabara hizo uzingatie usalama wa waenda kwa miguu na Baiskeli kwa kuwatengea njia yao.
Naye, Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila amewahakikishia wajumbe wa Kamati ya PAC kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kuisimamia TARURA ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Wakati huo huo Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa TARURA itazingatia na itaufanyia kazi ushauri wa Kamati uliotolewa ambao ni mzuri na utaboresha utendaji kazi wa TARURA.