Na MWANDISHI WETU
-ARUSHA
KATIKA kile kikachoonekana kuisuka upya Serikali yake ya Awamu ya Sita, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwelekeo wa namna anavyotaka Serikali yake iende huku akiwaonya mawaziri na makatibu wakuu kuhusu suala la maadili ya uongozi.
Pamoja na hali hiyo pia ameonya kitendo cha baadhi ya mawaziri wa Serikali yake kuajiri maofisa habari binafsi huku wakishindwa kuwatumia wale walioajiriwa na Serikali kwa ajili ya kutangaza taarifa na mafanikio ya Serikali kupitia wizara zao.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa hotuba yake katika mkutano wa faragha na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).
Kutoakana na hali hiyo Rais Samia amewataka mawaziri kuwajibika katika kujibu upotoshaji unaojitokeza kuhusu taarifa za Serikali.
Sambamba na hili pia amezitaka wizara kujibu kauli za upotoshaji zinazotolewa na wanasiasa kuhusu utendaji wa Serikali.
Katika kulitekeleza hilo, amewataka mawaziri kuacha kuajiri maafisa habari binafsi, badala yake wavitumie vitengo vya habari kutoa taarifa za Serikali.
Agizo lake hilo kwa wizara linatokana na kile alichokitolea mfano kuwa, amewahi kuibuka mwanasiasa aliyeikosoa Serikali kutumia fedha nyingi kutafuta vyanzo vipya vya maji, ilhali kuna visima kadhaa vilishachimbwa.
Mkuu huyo wa nchi alisema kuwa wizara inayohusika na hilo, ilipaswa kusimama haraka na kutolea ufafanuzi kuhusu hilo, badala ya kusubiri taarifa za upotoshaji zisambae.
“Nimewahi kuona kiongozi wa kisiasa akiilaumu Serikali inatumia fedha nyingi kutafuta vyanzo vipya vya maji kupeleka kwa wananchi, ilhali kuna visima kadhaa vilichimbwa nyuma na serikali iliviacha.
“Wizara inayohusika na hili, ilipaswa kusimama haraka kujibu kutoa facts (ukweli), fugures (takwimu) na kumueleza kwanini visima hivyo viliachwa na kwamba vimeachwa au havikuachwa,” alisema Rais Samia
Mkuu huyo wa nchi alisema kuwa visima vilivyotajwa na mwanasiasa huyo ndiyo vilivyoisaidia Dar es Salaam wakati wa changamoto ya ukame.