Na VERONICA SIMBA
-REA, HANDENI
BODI ya Nishati Vijijini (REB) imefanya ziara katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni yaliko makazi mapya ya wananchi wanaoendelea kuhamia kwa hiari kutoka Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, ambapo ahadi kutoka pande mbalimbali zimetolewa katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa ipasavyo.
Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, aliyeongeza Msafara huo Machi 26, 2024 ameahidi kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaosimamiwa na Bodi hiyo, utatekeleza kikamilifu, jukumu lake la kupeleka nishati ya umeme kwa wakazi wa eneo hilo ambalo hadi sasa linaendelea vizuri.
“Wakandarasi wetu wako eneo la kazi na tutahakikisha tunatekeleza kikamilifu kazi yetu kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza.
Aidha, Balozi Kingu amesema jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa na wadau wote wanaohusika katika zoezi hilo ni ushirikiano ili azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan iweze kutimia.
“Sote tushirikiane na sote tupeane taarifa kwa wakati. Naamini itawezekana iwapo sote tutaunganisha nguvu kwa pamoja,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando ameahidi kuwa yeye pamoja na viongozi wenzake watahakikisha vifaa vyote vinavyotumika katika kutekeleza mradi wa upelekaji umeme katika eneo hilo vinabaki salama.
Amesisitiza kuwa, hawataruhusu wala hawatakuwa tayari kuona kifaa chochote kikipotea au kutumika vibaya huku akitolea mfano tukio lililotokea siku chache zilizopita ambapo alisema baadhi ya watu waliojaribu kuiba vifaa vya mradi walikamatwa na wanaendelea kushikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Nimemwelekeza Mwendesha Mashtaka pamoja na OCD kwamba tutaifishe gari na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyehusika na tukio hilo ili iwe fundisho kwamba vifaa vinavyokuja kwenye miradi ya umeme usithubutu kugusa,” amesema DC Msando
Msando ameiahidi Bodi ya Nishati Vijijini kuwa endapo watajitokeza watu kushirikiana na wahalifu wa aina hiyo, ofisi yake haitasita kuwachukulia hatua ili malengo ya REA na Bodi yaweze kufikiwa.
Naye Kaimu Kamanda wa Operesheni, Luteni Kanali Edward Mwanga, pamoja na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na REA katika kupeleka umeme eneo hilo, pia ameiahidi Bodi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha miradi ya umeme inatekelezwa kikamilifu.
Katika pongezi zake, ametoa shukrani kwa REA kufikisha umeme eneo la kuzalishia tofali ambapo ameeleza kuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji zilizokuwa zinatokana na matumizi ya jenereta.
“Tunapofyatua tofali kwa kutumia jenereta, gharama zinakuwa kubwa sana, hivyo kuwepo kwa umeme kumepunguza gharama za mradi,” amefafanua.
Wakala wa Nishati Vijijini imekuwa ikitekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika kijiji cha Msomera ambapo ujenzi wa Mradi umekamilika kwa asilimia 100 kwa wigo wa awali na jumla ya shilingi bilioni 3.7 zimetumika kugharamia Mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Aidha, usambazaji wa umeme Awamu ya Pili ya ujenzi wa nyumba 5,000 Msomera umekamilika kwa asilimia 100 katika hatua ya kwanza inayohusu kupeleka umeme wa msongo wa kati (killovoti 33) kwa umbali wa kilomita 12.9 eneo la Kitalu F ambapo matayarisho ya vifaa vya ujenzi kama vile kufyatua tofali na utengenezaji wa vifaa vya chuma yatakuwa yakifanyika. Kazi hii imetekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 6.5
Mkandarasi M/S China Railway Construction and Electrification Bureau Group Company Ltd atatekeleza Mradi huu kwa gharama ya shilingi bilioni 14.2
Bodi ya Nishati Vijijini iko mkoani Tanga kushiriki vikao kazi na hivyo inatumia fursa hiyo kutembelea baadhi ya miradi ya nishati vijijini inayotekelezwa mkoani humo.