*YAIMARISHA UKAGUZI BANDARINI, VIWANJA VYA NDEGE NA MIPAKANI,SERIKALI YA RAIS SAMIA YAPELEKA SHILINGI MILIONI 250 KUSAIDIA UBORA BIDHAA ZA WAJASIRIAMALI
Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeweka wazi mikakati yake ikiwamo kuendelea kudhibiti ubora wa bidhaa zinazingia nchini kwa lengo la kulinda afya za wananchi.
Hayo yamesema leo Aprili 15, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha Wahariri kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina nchini (TR).
Akieleza kuhusu ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi amesema kuwa “TBS hudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje kwa kutumia mfumo wa Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC) pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini (Destination Inspection).
“Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shehena 100,851 kabla hazijaingizwa nchini sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083. Pia, jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417,”amesema Dk. Ngenya.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa TBS hudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje kwa kutumia mfumo wa ‘Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC)’ pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini (Destination Inspection).
GAWIO SERIKALINI
“Pamoja na yote tunatoa gawio kwa Serikali ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, TBS tumeweza kutoa gawio kwa Serikali Shilingi bilioni 18, lakini pia tumeweza kupata mapato ghafi bilioni 237 ndani ya miaka hiyo mitatu.
“… kwa hiyo hatuko nyuma, unajua Serikali ina miradi mingi na mikakati ambayo inahitaji fedha, kwa mfano ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge, bomba la mafuta, Bwawa la Nyerere ambalo sasa hivi tunapata umeme kidogo na wa uhakika, tunajua kwamba serikali yetu ina miradi mingi, kwa hiyo pamoja na kidogo tunachopata basi tunakata asilimia fulani kusaidia kule kuhakikisha mambo hayalali yanaenda,” amesema Dk. Ngenya.
UJENZI WA MAABARA
Akieleeza mkakati wa Shirika hilo, Dk. Ngenya, amesema kuwa wanatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Kanda ya Kaskazini (Arusha), ambapo kwa Maabara ya Kanda ya Ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa sita (6) ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Mkurugenzi huyo wa TBS amesema maabara ya kanda ya Kaskazini inatarajiwa kuhudumia mikoa minne ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
“Shirika linatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika kanda ya Ziwa (Mwanza) na kanda ya kaskazini (Arusha). Maabara ya kanda ya ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa sita ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu. Aidha, maabara ya kanda ya Kaskazini inatarajiwa kuhudumia mikoa minne (4) ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Katika hatua nyingine amesema Shirika limetengeneza mifumo ya kielektroniki inayotumika kutoa huduma zake na uanzishwaji wa mifumo ya kielektroniki imewezesha wateja kupata huduma za TBS popote walipo kwa wepesi na haraka hivyo kupunguza gharama kwa wateja.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya viwango 1,721 vya kitaifa viliandaliwa sawa na asilimia 101.2 ya lengo la kuandaa viwango 1,700. Viwango hivyo viliandaliwa katika nyanja mbalimbali.TBS imeshiriki katika uandaaji wa viwango vya kibiashara vya Afrika Mashariki na Afrika nzima,” amesema
NEEMA KWA WAJASIRIAMALI
Kuhusu utoaji wa leseni za alama ya ubora, Dk. Ngenya, amesema Serikali kwa kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya milioni 250 kwa dhumuni la kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.
“Katika hili ninapenda sana kumshukur Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka mitatu, imeweza kuteng fedha kupitia TBS ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000. Kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa bure na kwa wajasiriamali wadogo.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya wadau 5,789 kutoka mikoa mbalimbali nchini walipewa mafunzo hayo. TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo (MSEs) na wazalishaji ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama na hatimaye kukidhi ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa,” amesema Dk. Ngenya
Amesema kwa kipindi cha miaka miaka mitatu, jumla ya shehena 100,851 kabla hazijaingizwa nchini sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083. Pia, jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417.
Jukumu Kuu la TBS ni kuratibu uandaaji wa viwango na kusimamia utekelezaji wake (shughuli za utayarishaji wa viwango na udhibiti wa ubora wa bidhaa zote pamoja na kusimamia usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi).
UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU
Amesema Shirika linatekeleza mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Shirika na maabara (Viwango House – Dodoma), ambapo maabara hiyo itahudumia mikoa mitatu (3) ya kanda ya kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na mikoa mingine ya karibu.